Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi Sh3.6 bilioni za kusomesha wataalam zilivyoibeba Muhimbili

85009 Mimba+pic Jinsi Sh3.6 bilioni za kusomesha wataalam zilivyoibeba Muhimbili

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imesema katika kipindi cha miaka minne imetumia  Sh3.6 bilioni kusomesha wataalamu wake katika nchi mbalimbali  kwa ajili ya kuwajengea uwezo lengo likiwa kupunguza rufaa za matibabu nje ya nchi.

Hilo limefanyika kutokana na huduma za kibingwa zilizoanzishwa katika hospitali hiyo ambazo ni kupandikiza figo, vifaa vya usikivu, tiba radiolojia, tiba ya saratani ya damu, uchunguzi wa magonjwa ya mfumo wa chakula, ini na magonjwa mengine.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Novemba 19, 2019 na mkurugenzi mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya hospitali hiyo kwa miaka minne tangu Rais John Magufuli alipoapishwa kuwa kiongozi mkuu wa nchi Novemba 5, 2015.

“Kipindi kile (mwaka 2015) kero zilizokuwepo kwa wananchi ni vipimo kutofanya kazi kama MRI na CT-Scan kutokana na kuharibika kwa muda mrefu.”

“Ukosefu wa dawa, wagonjwa waliokuwa wakilala chini kupewa vitanda, kulipa stahiki za wafanyakazi ikiwemo posho na nauli za likizo,” amesema.

Amesema, “Rais (Magufuli) alitoa maagizo kuwa Muhimbili ianze kutoa huduma za ubobezi ili kupunguza rufaa za nje ya nchi, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi pamoja na kununua na kukarabati vitendea kazi na hapo ndipo tulianza kusomesha wataalamu ili kupunguza gharama.”

Amesema katika kipindi cha miaka minne wagonjwa 558 wamepewa huduma ya kibingwa ya tiba radiolojia na kati yao 274 walikua na uvimbe. Amesema walitibiwa kwa  Sh2.1 bilioni sawa na Sh8 milioni kwa mgonjwa mmoja.

Amebainisha kama wangepelekwa nje ya nchi kutibiwa ingeigharimu Serikali Sh26.3 bilioni sawa na Sh96 milioni kwa mgonjwa mmoja kwa safari nne zinazohitajika , “hapo Serikali imeokoa Sh24.1 bilioni kwa kutoa huduma hizi nchini.”

“Kwa upande wa upandikizaji figo wagonjwa 51 wamenufaika kwa gharama ya Sh1.5 bilioni ikiwa ni Sh30 milioni kwa kila mgonjwa na iwapo wangeenda nje ya nchi Serikali ingetumia Sh6.1 bilioni sawa na Sh120 kwa kila mgonjwa na kuokoa  Sh4.5 bilioni.”

Pamoja na mambo mengine, Profesa Museru amesema jumla ya uwekezaji uliofanyika ni Sh37.4 bilioni kwa kipindi cha miaka minne.

“Hii ni katika ununuzi wa vifaa tiba na mashine Sh23.7 bilioni, uboreshaji miundombinu Sh10 bilioni pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu Sh3.5 bilioni,” amesema.

Amesema kutokana na kusomesha wataalamu hao, Muhimbili imeokoa Sh4.5 katika upandikizaji figo, Sh2 bilioni upandikizaji vifaa vya kusikia, Sh1.3 bilioni huduma ya mfumo wa chakula na ini

na Sh24.1 bilioni katika tiba radiolojia. Amesema  Sh32 bilioni zimeokolewa kama wagonjwa wangepewa rufaa kwenda nje ya nchi.

Chanzo: mwananchi.co.tz