Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Je wajua haya ni mazoezi mepesi pia?

10358 Shita+Samweli TanzaniaWeb

Mon, 6 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jamii inahimizwa kufanya mazoezi ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza Non-communicable Diseases (NCDs) ukiwemo ugonjwa wa moyo, kisukari, kiharusi, figo na unene.

Ikumbukwe mazoezi mepesi yakiwemo ya kutembea, kukimbia, kuogelea na kucheza muziki wa haraka ni moja ya nyenzo rahisi ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Badala ya kwenda vituo vya mazoezi kulipia yapo mambo tunayofanya katika maisha ya kila siku pasipokujua ni mazoezi mepesi yasiyokuwa rasmi yanayoushughulisha mwili kimazoezi.

Upo utamaduni, hulka na tabia mbalimbali zisizozumgumziwa katika jamii ambazo watu hufanya katika maisha ya kila siku na kufanya mwili kujishughulisha na kuchoma sukari, mafuta ya mwilini.

Nikianza na utamaduni wa wafugaji ambao wana kawaida ya kutembea na kuswaga mifugo umbali mrefu kutafuta malisho.

Mtindo huu umewafanya kubeba tabia ya kupenda kutembea hata wanapofika mjini hutembea umbali mrefu, mfano mzuri ni jamii ya kabila la Kimasai.

Kabila la Masai ambalo lipo zaidi maeneo ya kaskazini ikiwemo Arusha na nchi jirani ya Kenya, wamekuwa wakionekana mjini wakitembea kwa miguu hata kama wana uwezo wa kukodi gari au kupanda usafiri wa daladala.

Kutembea ni mtindo bora kwa maisha kwa kuwa ni zoezi rahisi ambalo linaushughulisha mwili kwa kuchoma sukari au mafuta ya mwili. Tafiti zinaonyesha zoezi la kutembea huwafanya watu kuishi muda mrefu.

Maeneo ya mikoa ya Tanga, Pwani, Morogoro, Mwanza na Shinyanga ni maeneo ambayo watuwengi wa kawaida hupenda kutumia baiskeli. Kuendesha baiskeli kwa matumizi ya kubeba abiria, mizigo na kusafiria kutoka eneo moja kwenda jingine mara kwa mara kila siku ni moja ya zoezi linalofanywa pasipokujua lina tija katika afya zetu.

Mazingira tunayoishi na kufanya shughuli zetu za kila siku mara kwa mara ikiwamo maeneo yenye miinuko kama vile Lushoto, Marangu, Ludewa, Uluguru na Mahenge hufanya miili kufanya zoezi.

Wakati wa uzalishaji mali katika maeneo haya wakazi wengi hujikuta wakipanda na kushuka katika milima kutoka eneo moja kwenda jingine hivyo miili yao kujishughulisha kwa mazoezi pasipokujua.

Watu wanaoishi visiwani, kando kando mwa Bahari ya Hindi na Kanda ya Ziwa kuogelea ni sehemu yao ya shughuli za uvuvi au burudani lakini kumbe kufanya hivyo mara kwa mara ni zoezi lenye tija kiafya.

Utaratibu ambao umewekwa na baadhi ya dini na madhehebu ambao wana utaratibu wa kusali kila siku au mara kwa mara huku waumini wakitembea umbali kidogo kuifuata nyumba ya ibada.

Mfano kama nyumba ya ibada ipo kilometa moja kutoka makazi ya waumini kama wakienda na kurudi tayari mtu anakuwa ametembea kilometa mbili, hivyo tayari amefanya zoezi. Mambo mengine yanayochangia kuupa mwili mazoezi ni shughuli za kilimo, biashara za kutembeza, kazi za viwandani, kusukuma matoroli ya mizigo, bustani za umwagiliaji, kucheza ngoma za utamaduni, ufugaji wa nyumbani na ubebaji mizigo.

Mitindo na mienendo ya maisha kama hii ni mizuri kwa afya zetu kwa kuwa yanafanyika kila siku angalau kwa wiki mara tano kwa muda wa dakika 30-45, mtu atakuwa amefanya zoezi lenye tija ambalo litamfanya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Hivyo kwa wale watakaoshindwa kufanya mazoezi mepesi wanaweza kuiga mambo haya kushughulisha miili yao.

Chanzo: mwananchi.co.tz