Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Japan yaipa Tanzania bil. 3.45/- kukabili utapiamlo

Ela.webp Japan yaipa Tanzania bil. 3.45/- kukabili utapiamlo

Wed, 20 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SERIKALI ya Japan imetoa Dola za Marekani milioni 1.5 (Sh. bil. 3.45) kwa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) kwa ajili ya kuunga mkono mradi wake wa miaka minne wa Boresha Lishe kwa maeneo ya vijiji vya Kanda ya Kati mwa Tanzania.

Mradi huo uliozinduliwa mwaka 2017 unalenga kuimarisha lishe kwa wanawake na watoto 30,000 kwa kuhamasisha mabadiliko chanya ya tabia za lishe, kuhimiza uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na ugawaji wa chakula lishe maalumu kwenye wilaya za Bahi na Chamwino kwa Mkoa wa Dodoma na wilaya za Ikungi na Singida Vijijini kwa Mkoa wa Singida.

“Kwa hapa Tanzania, Serikali ya Japan imekuwa ikitoa misaada kwa sekta mbalimbali,” anaeleza Goto Shinichi, Balozi wa Japan nchini Tanzania.

“Mchango huu maalumu umetolewa kwa ajili ya wanawake na watoto wa vijijini, kwa ajili ya kuunga mkono kaulimbiu ya ‘Hakuna kumwacha mtu nyuma’ ya Mpango wa Maendeleo Endelevu wa 2030 kwa kuzingatia dhana ya msingi ya usalama wa mwanadamu. Msaada huu utasaidia kuboresha lishe na kuongeza kipato kwa makundi haya maalumu.

Taarifa iliyotolewa na WFP kwa vyombo vya habari jana, ilisema mradi wa Boresha Lishe unajikita kwenye kuongeza uelewa kuhusu; masuala ya lishe, upatikanaji wa vyakula mchanganyiko na usafi wa maji, mtu binafsi na mazingira (WASH).

Mradi pia unajengea uwezo jamii wa namna ya kuongeza uhakika wa lishe na chakula kwenye kaya kwa kufuga wanyama wadogo, kulima mazao mchanganyiko na kuwaunganisha kinamama kwenye vikundi vya Kuweka Akiba na Kukopa Vijijini (Vicoba), ili kusaidia upatikanaji wa mitaji.

Kwa ushirikiano na Japan, WFP inasambaza na kuweka vibanda vya huduma za umeme wa jua kwa vikundi 40 vya Vicoba vinavyosimamiwa na mradi huo. Vibanda hivyo vinatoa huduma za kuchaji simu na vifaa vingine vya umeme kwa malipo kidogo, na hivyo kuongeza kipato kwa Vicoba na wanachama wake.

“Kwa kupitia mradi wa Boresha Lishe, WFP inatumia mbinu ya sekta jumuishi kwa kugawa chakula lishe maalumu na kuhimiza mabadiliko chanya ya tabia za lishe huku ikiwawezesha wanajamii kuwa na shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa ajili ya kuwaongezea kipato,” anaeleza Michael Dunford, Mwakilishi Mkazi wa WFP Tanzania. “Kutokana na msaada wa serikali ya Japan, WFP inaimarisha lishe ya watoto na kutengeneza mustakabali mzuri wa baadaye wa jamii kwa ujumla.”

Vile vile, ili kufanikisha kusambaza na kujenga vibanda vya kutolea huduma za umeme wa jua, WFP inafanya kazi kwa karibu na kampuni binafsi ya Kijapani, kwa lengo la kunufaika na utaalamu walionao katika kuendesha biashara hiyo kwa miaka mingi. Mradi wa Boresha Lishe unafadhiliwa na Serikali ya Japan, Umoja wa Ulaya na WFP.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live