Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohammed Janabi amesema asilimia 90 ya wagonjwa wa figo wasioweza gharama hospitali binafsi wanahudumiwa hapo.
Janabi amesema hayo leo Jumapili Julai 9, 2023 katika mbio za 'Figo Marathon' zilizofanyika katika Viwanja vya Mnazimmoja jijini hapa zilizoandaliwa na Taasisi ya Healthier Kidney Foundation (KHF) kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa lengo la kukusanya fedha za kusaidia wagonjwa wanaofanya huduma ya kuchuja na kusafisha damu katika hospitali hiyo.
Amesema katika kila wanawake wanne, mmoja ana tatizo la figo na kwa upande wa wanaume, kati ya watano mmoja ana tatizo hilo, huku akisema kuwa asilimia kubwa la tatizo la figo linasababishwa na shinikizo la juu la damu.
"Tatizo la figo ni kubwa na tunafanya usafishaji wa wagonjwa wa figo wastani watu 150 kwa siku na wanaingia kwa awamu tatu huku kundi la mwisho likimaliza huduma saa moja usiku," amesema Janabi.
Janabi amewataka watu kuwa na pensheni ya bima ya afya ili kuwasaidia katika magonjwa kwani asilimia 40 wanaopata maradhi ya figo hawana uwezo wa kulipa gharama za usafishaji.
"Kumsafisha mgonjwa wa figo anatakiwa kulipa Sh 180,000 kwa awamu na ikitokea umepangiwa awamu tatu kwa wiki ni gharama kubwa,"amesema Janabi.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyekuwa mgeni rasmi katika mbio hizo amesema watu wasisubiri mbio za Figo marathon ili kufanya mazoezi bali iwe ni utamaduni wa kufanya hivyo na kuendelezwa kwa elimu za mazoezi kwa wote.
Chalamila amewataka watu kuacha tabia ya kunywa dawa kiholela bila maelekezo ya madaktari ili kuepukana na maradhi yatakayoathiri figo.
"Tusipuuze aina za mazoezi, ulaji wetu na yale yote ambayo tunaelekezwa na madaktari kuyafanya ili kuepukana na maradhi mbalimbali,"amesema Chalamila