SERIKALI imeitaka jamii kuhakikisha watoto wanapata chanjo kipindi hiki chenye maambukizi ya virusi vya corona (Codid-19) ili wapate kinga ya magonjwa mengine.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Watoto, Dk. Ahmad Makuwani, kwenye semina ya waandishi wa habari wa mikoa ya Singida na Dodoma kuhusu chanjo.
Alisema maambukizi ya corona kwa sasa yamepungua na kuwataka Watanzania kutotumia ugonjwa huo kama sababu ya kutowapeleka watoto kupata chanjo.
“Tulikuwa tunaenda vizuri, lakini hivi karibuni idadi ya watoto na wasichana wanaopaswa kupata chanjo ya mlango wa kizazi imepungua, hizi chanjo ni muhimu sana jamii ipeleke watoto kwenye vituo wapate chanjo,” alisema.
Alisema Tanzania imepiga hatua kwa sasa katika utoaji wa huduma za chanjo, huku akidai kuwa kuna vituo zaidi ya 6,000 vinavyofanya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.