Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jafo asifu barabara Hospitali ya Uhuru

3c5979af5befbeee2af27abb29ffe204 Jafo asifu barabara Hospitali ya Uhuru

Sat, 6 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara inayoingia Hospitali ya Uhuru kwa kiwango cha lami yenye urefu wa mita 320 kwa njia mbili.

Barabara hiyo inayosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Alitoa pongezi hizo juzi alipokagua miradi mbalimbali mkoani Dodoma. Alisema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo.

“Tumejenga Hospitali ya Uhuru lakini sehemu hii ya kuingilia ilikuwa na changamoto kubwa, nimekuja hapa kuangalia maendeleo ya ujenzi wa barabara hii na kwa kweli nimeridhika kuona maendeleo ya ujenzi wa barabara hii,” alisema Jafo.

Alimtaka mkandarasi anayejenga barabara hiyo, Kampuni ya Nyanza, kutumia muda uliopo kukamilisha mradi huo kwa wakati kutokana na changamoto za mvua zinazoendelea kunyesha.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Tarura Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Nelson Maganga alisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami umefikia asilimia 85 na tayari lami nyepesi imekamilika kwa ajili ya kuweka tabaka la lami nzito.

“Ujenzi wa barabara umefikia asilimia 85 kukamilika na tunatarajia mkandarasi kumaliza kazi kulingana na mkataba kufikia Machi 14, mwaka huu sehemu hii ya barabara imegharimu kiasi cha shilingi milioni 511,” alisema Nelson.

Katika hatua nyingine, Jafo alikagua ujenzi wa barabara za Mji wa Serikali eneo la Mtumba kwa kiwango cha lami, zenye urefu wa kilometa 51.2 na kuonesha kutoridhishwa na kasi ya mkandarasi anayetekeleza ujenzi huo, Kampuni ya China Heinan International Cooperation (CHICO). Alimtaka mkandarasi huyo kumaliza ujenzi kama ilivyo kwenye mkataba ifikapo Julai 30, 2021.

“Sijaridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huu kuwa chini ya asilimia 6, leo hii mpo asilimia 63 na mlitakiwa muwe asilimia 69, mimi nilikuja hapa nikijua mpo asilimia 70, sihitaji mjadala wa aina yeyote ninachotaka mradi huu uwe umekamilika kama ilivyo kwenye makubaliano,” alisema Jafo.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa barabara za Mji wa Serikali, Mtumba, Mkurugenzi wa Barabara za Mijini Tarura, Mohamed Mkwata alisema kuwa mkandarasi amefikia asilimia 63 za maendeleo ya jumla ya utekelezaji wa mradi na alitakiwa kuwa asilimia 69. Alisema kuwa tabaka la lami ujenzi umefikia kilometa 11.2, uwekaji wa lami nyepesi kilometa 15.7, ujenzi wa tabaka la pili umefikia kilometa 15.7, ujenzi wa tabaka la kwanza umefikia kilometa 15.7, ujenzi wa mifereji kilometa 6.6 na vivuko vilivyojengwa ni 64 kati ya 130 vinavyohitajika.

Mkwata alieleza kuwa katika kipindi cha mwezi Novemba mwaka jana, uhaba wa saruji na mvua zinazoendelea kunyesha, vilisababisha baadhi ya kazi kusimama hivyo kufanya mkandarasi kuwa nyuma kwa asilimia sita za utekelezaji wa mradi.

Alisema kuwa ili kufidia muda uliopita, mkandarasi aliongeza mitambo ili kumaliza mradi huo kwa wakati uliopangwa. Mradi huo unatarajiwa kukamilika Julai 30, mwaka huu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz