Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JKCI yaonya ongezeko la matatizo ya moyo

91ee9bf3a6d3530d0d035ee949f2ddff JKCI yaonya ongezeko la matatizo ya moyo

Tue, 6 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ya Dar es Salaam imesema wagonjwa wanaofi ka kliniki ya hospitali hiyo kwa siku ni 200 hadi 400. Habari zinasema kwamba kwa takwimu hizo tatizo la magonjwa ya moyo nchini ni makubwa.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka JKCI, Dk Samwel Rwehemamu alisema hayo alipokuwa akiuelezea ugonjwa huo katika maadhimisho ya siku ya moyo ulimwenguni.

Dk Rwehemamu alisema taasisi ilianza rasmi mwaka 2013 ambapo walikuwa wakiona wagonjwa wachache lakini kwa kadri siku zinavyoendelea wagonjwa wamekuwa wakiongezeka.

“Tangu tumeanza tunaona karibu asilimia 60 hadi 70 ya wagonjwa wa shinikizo la damu, wengi waliobakia ni wagonjwa wenye shida ya mishipa ya damu kuziba ambayo mishipa inayosambaza damu kwenye moyo inaziba hivyo inasababisha kifua kuuma.

Vilevile wagonjwa wa moyo wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wanaongezeka kila siku, kwa mfano mishipa ya moyo ikiziba inahitaji upasuaji ili kuzibua, pia wanaohitaji uchunguzi wa mishipa ya moyo wanaongezeka.

“Kwa mfano mwaka jana mpaka Desemba tulichunguza wagonjwa 1,000,” alisema. Daktari bingwa huyo alisema kwa Dar es Salaam ni kama asilimia 30 wana shida ya shinikizo la damu, kwani mtu anapokuwa na shinikizo la damu mishipa ya moyo huweza kuziba hivyo kuhitaji kuzibuliwa.

Kwa maelezo yake utafiti uliofanyika Simanjiro unaonesha kwamba asilimia 28 walikutwa na matatizo hayo, vilevile Mafia walikuwa asilimia kati ya 25 mpaka 30.

Alisema pia mwishoni mwa mwaka 2018 walifanya utafiti katika Hospitali ya Songea ambapo waliona wagonjwa 800, asilimia 70 ya wagonjwa walikuwa na shinikizo la damu hivyo waliwashauri wafike katika kliniki ya JKCI ili waendelea na matibabu.

“Kwa mfano tulifanya utafiti Tanga mwaka 2018 tulikuta watu waliokuwa na shinikizo la damu wengi walianzia miaka 65 kwenda juu, lakini uzito mkubwa ulikuwa kwa wanawake.

“Uzito mkubwa pia ni shida kubwa ya kuleta matatizo ya damu. Pia ukiangalia chini ya miaka 18 wengi uzito umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Ukiwa na uzito mkubwa mwanzoni mwisho wake utakuwa na matatizo ya ugonjwa wa moyo, pia kisukari na ukishakuwa na kisukari inasababisha pia kuwa na matatizo ya moyo unaweza kupanuka mishipa ikaziba kutokana na hali ya maisha,” alisema.

Alisema mtu ana uamuzi wa kuepuka kuwa na magonjwa hayo yasiyoambukiza kwa kuwa na mfumo unaofaa wa maisha ili kuepuka gharama za matibabu ambazo ni kubwa kwani kutibu shinikizo la moyo au mishipa ya moyo iliyoziba ni gharama kubwa.

“Kwa hiyo life style (mfumo wa maisha) tuliyonayo inachangia kwa vijana kupata shida kwani unaona ulaji wa chipsi mayai ni kwa wingi sana, wakina dada mnapenda chipsi kuliko vijana wa kiume mwisho uzito unaongezeka sana moyo unakuwa kwenye hatarishi,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz