Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JKCI yafunga mtambo mfumo wa umeme wa moyo

Ddbf134219289c6ec76bb61716135939.jpeg JKCI yafunga mtambo mfumo wa umeme wa moyo

Sun, 2 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imefunga mtambo wa kisasa wenye thamani ya Sh bilioni 4.6 wa uchunguzi na matibabu ya moyo uliounganishwa na mtambo wa wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo.

Fedha za kununua mtambo huo ambao umefungwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), zilitolewa na serikali mwanzoni mwa mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema mtambo huo umeshaanza kutumika.

Alisema licha ya kutibu mfumo wa umeme wa moyo pia utafanya uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo, kuweka vifaa visaidizi vya moyo pamoja na kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba.

“Tunaishukuru serikali kwa kuiwezesha JKCI na kufunga mtambo huu wa kisasa ambao una uwezo wa kufanya uchunguzi na kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo,” alisema.

Aliendelea, “Kufungwa kwa mashine hii yenye teknolojia ya hali ya juu kutaweza kuokoa maisha ya watu wengi wenye matatizo ya moyo ikiwamo mfumo wa umeme wa moyo. “

Alisema wanao wagonjwa wengi ambao mfumo wa umeme wa moyo umekuwa haufanyi kazi vizuri ikiwa ni pamoja na hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yake ya moyo yanakwenda haraka kuliko kawaida.

Mkurugenzi huyo mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, alisema kupitia utaalamu wanaoendelea kuupata kutoka kwa wenzao wa nchi za nje ambao wamewatangulia katika matibabu ya moyo pamoja na kusimikwa kwa mtambo huo wataweza kuwatibu wagonjwa hao nchini

“Kwa upande wa wataalamu tunao wa kutosha kwani kuna ambao tumewasomesha nchini China na Afrika Kusini,” alisema.

Vile vile alisema kupitia kambi mbalimbali za matibabu ya moyo ambazo wanazifanya kwa kushirikiana na wenzeo wa nje ya nchi wenye utaalamu mkubwa zaidi yao kuwasaidia kupata utaalamu wa kutosha na wa kisasa.

Kwa upande wake, Hassan Ally kutoka kampuni ya Biosense webser ambao ndiyo wafungaji wa mtambo huo, alisema katika nchi za Afrika ya Mashariki mtambo huo ni wa pili kufungwa. Wa kwanza ulifungwa katika Hospitali ya Aga Khan iliyopo Mombasa nchini Kenya.

Alisema mtambo huo una teknolojia mpya na ya kisasa ambayo hivi sasa inafanyika katika matibabu ya moyo duniani. Alitaja nchi nyingine ambazo zimefunga mtambo huo katika Afrika ni pamoja na Afrika ya Kusini na Misri.

Daktari mwanamke pekee nchini ambaye ni mtaalamu mbobezi wa moyo na mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa JKCI, Honoratha Maucky alisema kufungwa kwa mtambo huo kutawasaidia kutoa huduma nyingi zaidi kwa wagonjwa na kuokoa maisha yao.

Dk Maucky alisema tatizo la mfumo wa umeme wa moyo ni moja ya magonjwa wanayokutana nayo kila siku hivyo kuwapo kwa mtambo huo kutawasaidia kutoa huduma kwa wakati kwa wagonjwa wenye matatizo hayo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz