Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JKCI ‘kutengeneza’ mabingwa wa moyo 11 kila mwaka

1c4883d5518be7df0343f8a141d03d49 JKCI ‘kutengeneza’ mabingwa wa moyo 11 kila mwaka

Thu, 22 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa kitivo mahususi cha ufundishaji wataalamu mabingwa wa moyo ndani ya nchi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), na inatarajia kila mwaka 'kutengeneza' wahitimu 10.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema hayo juzi alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao cha nne cha Baraza la Wafanyakazi wa taasisi hiyo.

Profesa Janabi alisema hatua hiyo itaisaidia Tanzania kupata wataalamu mabingwa wa moyo, watakaosaidia kuendelea kuimarisha huduma za matibabu hayo nchini.

“JKCI ni taasisi pekee kubwa ya umma inayotoa matibabu haya nchini, lakini hii si hospitali tu, imekuwa pia sehemu kubwa ya mafunzo kwa madaktari na wauguzi, kwa kuwa sisi si chuo, ndiyo maana tunashirikiana kwa ukaribu na MUHAS, mwaka huu watahitimu wataalamu saba na kuanzia mwaka ujao wa masomo tunatarajia watahitimu wataalamu kumi,” alisema Profesa Janabi.

Aliongeza, “Kwa mfano hizi digrii za pili za uzamili kwa mfano 'masters in cardiology' ya miaka miwili, asilimia 96 ya walimu wanatoka JKCI kwa ushirikiano na MUHAS tunatoa hizi kozi.

“Kuna kozi mpya ya upasuaji wa kifua ambayo imeanzishwa walimu sita kati ya wanane wanatoka JKCI ni hatua kubwa ambayo taasisi imepitia kuwa kitivo cha 'uzalishaji' wataalamu mabingwa wa moyo nchini.”

“Zaidi ya asilimia 90 ya wataalamu mabingwa wa moyo nchini hivi sasa wapo JKCI, uwiano kwa nchi zetu zote Afrika bado si mzuri, kwa mfano sisi ndiyo hospitali kubwa kuliko zote si tu Tanzania bali katika Ukanda wote huu wa Afrika Mashariki na Kati,” alisema Profesa Janabi.

“Juhudi zimefanyika kubwa sasa hivi Dodoma (Hospitali ya Benjamin Mkapa - BMH) imeanzisha Kitengo cha Moyo tunashirikiana nao kwa ukaribu vile vile Hospitali ya Rufaa ya KCMC nayo imeanzisha kitengo na tunafanya nao kazi kwa ukaribu,” alibainisha.

Aliongeza, “Hivyo kila mwaka Tanzania tunatarajia tutazalisha madaktari kati ya 10 na 13, hii ni namba kubwa mno.”

Kuhusu baraza hilo la wafanyakazi, Profesa Janabi ambaye pia ni Mwenyekiti wake alisema limekuwa la mafanikio likiwaunganisha uongozi wa juu na wafanyakazi kufahamu huduma wanazotoa, changamoto na wapi wanaelekea. Lina wawakilishi 62 kutoka kila idara.

“Tunajivunia utulivu mkubwa uliopo kwenye baraza hili, menejimenti inaongoza wafanyakazi 310 na wote wanahitaji kupata huduma wanazostahili ili wananchi wapate huduma ambazo nchi inafikiria kuzitoa kwao,” alieleza.

Katibu wa baraza hilo, Dk Samwel Rweyemamu alisema limekuwa likisimamia kwa dhati maslahi ya wafanyakazi ili kuimarisha morali ya utendaji kazi kwa maslahi mapana ya wananchi wanaowahudumia.

“Kwa mfano, kila mwaka tumekuwa tukitambua mfanyakazi bora, tumependekeza pia iwe wafanyakazi watatu bora kila mwaka, yaani mshindi wa kwanza, pili na tatu ili kuwapa motisho na hamasa wafanyakazi kuendelea kufanya vema zaidi,” alibainisha Dk Rweyemamu.

Chanzo: habarileo.co.tz