Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Italia yatoa bilioni 3.4/- sekta ya afya

ITALYTZ Italia yatoa bilioni 3.4/- sekta ya afya

Sat, 4 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI ya Italia imetoa msaada wa manufaa wa Euro 1,250,000 kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya nchini.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jana, ilisema ujumbe wa wataalamu wa afya kutoka Italia umewasili jana kwa ziara maalumu ya kutathimini na kufahamu mahitaji na vipaumbele vya Tanzania katika sekta ya afya kwa hospitali zilizopo nchini.

Ilisema hatua hiyo imetokana na Serikali ya Italia kutenga kiasi cha Euro 1,250,000 (takriban Sh bilioni 3.44 kwa viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni jana) za msaada wenye manufaa kwa Tanzania hali iliyoufanya ujumbe wa madaktari watatu kufanya ziara kuanzia Septemba 3 hadi 12, mwaka huu, kwa ajili ya kukutana na uongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kuainisha mahitaji na vipaumbele vitakavyoweza kufadhiliwa kwa fedha hizo katika sekta ya afya.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ujumbe huo unaongozwa na Dk Davide Bonechi aliyefuatana na Dk Giulia Dagliana na Dk Beatrice Borchi ambao wote ni madaktari kutoka Kituo cha Taifa la Italia cha Afya Duniani.

Tanzania imekuwa ikishirikiana na Italia katika miradi mbalimbali ya afya nchini, na ushirikiano rasmi katika sekta ya afya ulianza mwaka 1968 kupitia Shirika la Madaktari wa Italia-CUAMM-Doctors with Africa.

Kuanzia wakati huo, Serikali ya Italia imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya afya kama vile miradi ya kupambana na utapiamlo, afya ya watoto wachanga, afya ya uzazi na kupunguza maambizi ya Virusi Vya Ukimwi.

Aidha, Italia imefadhili miradi ya usafi wa mazingira jijini Dodoma na pia katika kuunga mkono jitihada za serikali katika utoaji wa huduma za afya.

Serikali ya Italia imekuwa ya kwanza kufungua Kituo cha Tiba ya Mifupa na Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza katika Hospitali ya St. Gaspar, Dodoma. Vituo hivyo, vinaendelea kutoa mchango mkubwa katika kuboresha afya ya wananchi wa Tanzania hususan wakazi wa Dodoma.

Chanzo: www.habarileo.co.tz