Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Islamic Help  yatoa bil 3/- ujenzi wa hospitali Handeni

D6979e9848c356e7a0654994e42b6d89.jpeg Islamic Help  yatoa bil 3/- ujenzi wa hospitali Handeni

Thu, 15 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHIRIKA la Islamic Help limetoa msaada wa Sh bilioni tatu kwa Halmashauri wa Wilaya ya Handeni kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa hospitali ya wilaya pamoja na ununuzi wa vifaa tiba na samani.

Hati za makubaliano ya msaada huo zimesainiwa jana baina ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Musa Mwanyumbu pamoja na Mkurugenzi wa shirika hilo, Amjad Khan mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Mkuu wa Mkoa Shigela alisema ujio wa msaada huo ni matokeo ya utekelezaji wa miradi kwa kutumia force account kwani umesaidia kudhibiti upotevu wa fedha lakini miradi kukamilika kwa wakati.

"Haya ndio matunda ya force account kwani miradi inatekelezwa kwa uwazi, hivyo hata hawa wadau wa maendeleo wameweza kuvutika kutoa fedha hizo ili kuharakisha ukamilishaji wa hospitali hiyo kwa wakati," alisema.

Alisema utaratibu huo ndio umewavutia Islamic Help kutoa fedha kwa halmashauri na kujenga jengo wenyewe badala ya wao wafadhili kuwajengea kwa gharama kubwa lakini baadaye matokeo yanakuwa madogo.

Aidha kwa upande wake Mkurungenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Handeni, William Makufwe alisema jumla ya Sh bilioni 2.4 zitakwenda kujenga majengo huku Sh milioni 600 zitanunua vifaa tiba na samani.

"Fedha hizo zitaweza kusaidia hospitali hiyo kutoa huduma kwa zaidi ya asilimia 60, hivyo wananchi wataweza kuanza kupata huduma wakati ambapo maeneo mengine yakitarajiwa kukamilika," alisema Makufwe.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Shirika la Islamic Help, Amjad Khan alisema shirika hilo lilikuwa limejikita katika kusaidia ujenzi wa miradi ya maji hususani katika maeneo ya vijijini ambayo yanakabiliwa na changamoto za uhaba wa maji.

"Tumeridhishwa na ushirikiano tuliopewa na serikali katika ujenzi wa miradi ya maji, hivyo tumeamua kujikita katika kusaidia ujenzi wa miundombinu na vifaa katika sekta za elimu na afya," alisema Khan.

Chanzo: www.habarileo.co.tz