Dar es Salaam. Licha ya kuwa elimu kuhusu Fistula imeendelea kutolewa kwenye jamii na kuelezwa kuwa ugonjwa huo unatibika, bado kuna wanawake wanachelewa kupata matibabu kwa sababu ya Imani za kishirikina.
Hayo yameelezwa na Theodora Masako ambaye ni muuguzi anayehudumia wagonjwa hao katika hospitali ya CCBRT wakati kwaya ya Kwaya ya Gethmane ya Kanisa la SDA (Wasabato) Mtaa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam ilipowatembelea wagonjwa hao na kuwapatia msaada.
Masako amesema kuwa kuna changamoto kubwa ya wagonjwa kupata matibabu kwa wakati wakihofia gharama za matibabu huku wengine wakihusisha ugonjwa huo na Imani za kishirikina.
"Tumekuwa tukitoa elimu kuhusu ugonjwa huu ambao hauna uhusiano na ushirikina, na wala matibabu yake hayana gharama yoyote ile na hapa kwetu tunatoa matibabu bila malipo. Nitumie fura hii kuishukuru kwaya hii ya Gethmane kwa kutambua umuhimu wa kutoa msaada wao kwa ajili ya wagonjwa hawa ambao tunawahudumia hapa hospitalini kwetu,"amesema Masako.
Amesema wagonjwa wanapoona wanatambelewa wanafarijika na kuwapa moyo kuwa wapo watu ambao wanawathamini na kuwajali kwani moja ya changamoto ya ugonjwa huo, wengi wao wamekuwa wakitengwa na jamii na wakati mwingine hata na familia zao.
Mwalimu wa kwaya hiyo Stella Malingoza amesema kuwa mwaka huu kwaya wanatimiza miaka 10 na wanajiandaa kuzindua DVD zao mbili Oktoba 13 hivyo wameona ni vema kabla ya kufanyika kwa uzinduzi wakatoa msaada huo ambao ni sabuni, mafuta ya kupakaa, dawa ya meno na mswaki.
Pia Soma
- Takukuru yamng’ang’ania hakimu kwa tuhuma ya kupokea rushwa
- Katavi-Rukwa yazidi kuunganishwa kwa lami
- KALAMU HURU: Waziri anapoomba msamaha kwa Rais, kwa wananchi kumchagua mpinzani
“Hivyo tumekuja CCBRT kwa ajili kuwaona mama zetu na dada zetu wenye kusumbuliwa na ugonjwa fistula na kadri tukavyopata tutarudi kwao na kwa wengine.Thamani vifaa hivi ni Sh2.4 milioni ,”
Kwa upande wake mchungaji wa kanisa hilo Masunya Athony amesema watu wanapokuwa wagonjwa si rahisi kwao kupata neno la Mungu kwa usahihi, hivyo kwa kutambua hilo wameona kanisa lao lina wajibu wa kuwafikia wagonjwa na kuzungumza nao ikiwa pamoja na kushiriki nao maombi.