Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ilichokisema Serikali ya Tanzania kuhusu virusi vya corona

97516 Pic+corona Ilichokisema Serikali ya Tanzania kuhusu virusi vya corona

Sat, 29 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy  Mwalimu  amesema hakuna aliyebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona nchini, kuwataka Watanzania kuacha kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa.

Ameeleza hayo leo Jumamosi  Februari 29, 2020 katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Amesema licha ya nchi 51 kuripoti wananchi wake kupata maambukizi, zikiwemo nchi tatu za barani Afrika, ugonjwa huo haujafika nchini.

Amesema ili kukabiliana na ugonjwa huo uliosababisha vifo vya watu zaidi ya 2,400 nchini China, wanafanya uchunguzi kufuatilia wasafiri  wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege na bandari.

“Kuanzia Januari 30 hadi Februari 27, 2020 wasafiri 11,048 wamechunguzwa katika mipaka yetu, hawa wametokea katika nchi zilizo na ugonjwa huu kwa sasa ikiwemo China,” amesema

Amesema wizara hiyo ina vipima joto 140, vikiwemo 125 ni vya mkono na vya kupima watu wengi kwa mpigo vikiwa 15.

Pia Soma

Advertisement

“Lakini pia tumeongeza idadi ya wataalamu wa afya katika maeneo ya mipakani, tumeajiri  watumishi 100 ili kuimarisha ufuatiliaji wasafiri wanaoingia nchini kupitia maeneo ya mipakani.”

“Pia Serikali imeimarisha uwezo wa kupima sampuli kupitia maabara yetu ya Taifa ya afya ya jamii kwa watu wote wanaohisiwa kuwa na viashiria au dalili za ugonjwa huu ambapo majibu hupatikana ndani ya masaa manne hadi sita,” amesema Ummy.

Amewataka Watanzania kuzingatia mambo mbalimbali yanayoweza kuwakinga na maambukizi ya virusi vya corona na angalau kwa muda kuachana na desturi za kusalimiana kwa kupeana mikono, kukumbatiana.

“Katika kipindi hiki ambacho ugonjwa wa corona unasambaa katika nchi tofauti walau tuepuke kusalimiana kwa kupeana mikono, kukumbatiana na kupigana mabusu.”

“Kama wizara inatoa siku tatu kwa kila mkoa kuhakikisha unawasilisha kwa katibu mkuu wa Wizara ya Afya jina la kituo ambacho kimetengwa maalumu kwa ajili ya kuhudumia washukiwa au wagonjwa endapo watatokea kila halmashauri,” amesema Ummy.

Mganga mkuu wa Serikali, Dk Mohammed Kambi amewataka Watanzania kuwa watulivu na kuacha kupotoshwa na taarifa zinazosambaa mtandaoni kuwa pombe inaweza kutibu virusi vya corona.

“Ni vyema kuzingatia na kuchukua tahadhali namna mnavyoweza kujikinga na ugonjwa huu na Watanzania wajenge tabia ya kusubiri taarifa rasmi na siyo za mtandaoni,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz