Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ijue sikoseli, epuka unyanyapaa

9c10ba70aebc789fe2fab4bb86747a63 Ijue sikoseli, epuka unyanyapaa

Thu, 10 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UGONJWA wa selimundu au sikoseli, kimsingi unarithiwa kutoka kwa wazazi ambao wana vinasaba vyenye seli hizo. Kwa hiyo wagonjwa wa selimundu hawaambukizi hata kwa damu yao kuongezewa mtu mwingine bali zaidi ya kurithi.

Hata pale wazazi wanapokuwa na vinasaba hivyo, uwezekano wa kuzaa watoto wenye ugonjwa huo ni nusu kwa nusu (asilimia 50), yaani nusu ya watoto wa familia hii ndio huwa na ugonjwa huo.

Hata hivyo, asilimia 25 wanaweza kupata na asilimia 25 nyingine wanaweza kuwa wasambazaji (carrier).

Daktari bingwa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, aliyebobea katika ugonjwa ya selimundu, Dk Stella Malangahe anasema, ugonjwa huo huwapata zaidi watoto wa chini ya miaka mitano baada ya kuurithi.

Dk Malangahe anayetoa huduma katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma anasema kutokana na jamii kutojua namna sikoseli inavyoambukiza, Kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wameamua kutoa elimu kwa umma kupitia mwezi wa Kuelimisha Jamii juu ya ugonjwa huo.

Kaulimbiu yake ni ‘Ijue Sikoseli na Epuka Unyanyapaa,’ inayoeleza wazi kwamba magonjwa yasiyoambukiza yameenea kwa kasi nchini hasa Kanda ya Ziwa pamoja na mkoa wa Kigoma.

“Hapa nchini wagonjwa wengi wa sikoseli wanatoka Kanda ya Ziwa katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Kagera, Mara, Simiyu na Kanda ya Magharibi hasa mkoa wa Kigoma.

Dk Malangahe anasema hata hivyo kwamba idadi ya wagonjwa wa sikoseli imeongezeka kwa kiasi kikubwa nchini. Kwa siku anasema anahudumia wagonjwa zaidi ya wawili, na wote wanaweza kuwa wanatoka Kanda ya Ziwa.

Anasema utafiti bado unafanyika ili kujua kwa nini tatizo la sikoseli linawakumba sana watu wa Kanda ya Ziwa.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2017, zinaonesha kwamba tatizo la sikoseli lipo duniani na Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye maambukizi ya vinasaba kutoka kwa wazazi kwenda kwa watoto kwa kiwango kikubwa.

Tanzania inashika nafasi ya tano duniani ikitanguliwa na Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), India, Angola, lakini pia ipo nafasi ya nne barani Afrika ukiondoa India ambayo ipo Bara la Asia.

Kwa takwimu hizo ni wazi, tatizo la sikoseli nchini ni kubwa, kwani kwa mwaka wanakufa watoto wa chini ya miaka mitano 11,000 kutokana na kuugua ugonjwa huo.

Utafiti wa WHO unaonesha kwamba kama ugonjwa huo hautadhibitiwa au hatua za makusudi hazitachukuliwa, kuna uwezekano mkubwa kuendelea kuongezeka kwa vifo vya watoto nchini kutoka takwimu za sasa hadi 22,000 ifikapo mwaka 2025.

Dk Malangahe anasema takwimu za WHO pia zinaonesha kwamba kila mwaka duniani wanazaliwa watoto wenye ugonjwa huo 300,000 na kwamba bila kuwa na jitihada za kuudhibiti, wagonjwa wanaozaliwa na vinasaba hivyo inaweza kuongezeka mara mbili ifikapo 2025.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, watu kati ya asilimia 15 hadi 20 duniani wanatembea na vinasaba vya sikoseli mwilini kwa kujua au bila kujua. Idadi hiyo anasema ni kubwa ambayo inataka hatua za makusudi za watu kupima ili kujua afya zao.

Dk Malangahe anasema, serikali haijakaa kimya, kuna jitihada zinafanyika za aina mbili; moja ni mkakati wa kuanza kupandikiza uloto au uboho kwenye mishipa ya mwili ili kuponya ugonjwa huo.

Upandikizaji huo anasema unaanza kufanyiwa majaribio katika hospitali mbalimbali nchini ikiwemo hospitali ya taifa Muhimbili, hospitali ya rufaa Benjamin Mkapa na Aga Khan.

Jitihada hizo anasema zikifanikiwa na kuonesha ufanisi, basi wenye sikoseli watakuwa wanatibiwa kwa njia hiyo ya kipandikizwa uboho au uloto.

Pamoja na jitihada za kupandikiza uboho kuendelea katika hospitali mbalimbali, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jami, Jinsia, Wazee na Watoto, imekuja na mkakati mwingine wa kutafuta dawa za kutibu ugonjwa huo.

Kutokana na teknolojia kukua duniani kuna dawa aina ya hydro-urea ambayo inaweza kutibu ugonjwa wa sikoseli na kupona kabisa. Dk Malangahe anasema dawa hiyo inapatikana katika Hospitali za Rufaa ikiwemo Muhimbili (Upanga), Benjamin Mkapa, KCMC na Muhimbili (Mlonganzila).

Anasema bei ya dawa hiyo iko juu lakini ili kupunguza gharama, wizara imefanya jitihada za kuingiza dawa hiyo kwenye utaratibu wa dawa za kutibiwa kwa bima ya afya.

Wizara tayari imeshafanya mawasiliano na Bohari ya Dawa (MSD) ili kuagiza dawa hizo ili zipatikane kwa wingi nchini. Je, mtu atajuaje kwamba anaugua sikoseli? Dk Malangahe anasema kuna dalili zake, kubwa zaidi ikiwa ni ukosefu wa damu mara kwa mara.

Sikoseli ambayo ni chembe nyekundu inayotengeneza protini kubadilika na kuwa nusu duara (sickle), huwa zinajibana kwa kushindwa kupita kwenye mirija ya damu na hivyo kusababisha maumivu mahali zilipokwama.

Maumivu huwa makali kutoka unywelini hadi kwenye vidole vya miguuni yanayosababishwa na seli hizo kukwama baada ya kubadilika kutoka duara hadi nusu duara (nusu mwezi) na hivyo kushindwa kupita.

Dk Malangahe anasema kulundikana pamoja bila kupita, licha ya kusababisha maumivu, husababisha pia maeneo mengine ya mwili kukosa chembechembe za damu nyekundu na hivyo kumletea mgonjwa upungufu wa damu mwilini.

Anasema seli hizo pia hufa haraka, hali inayosababisha upungufu wa damu mwilini na hivyo mtoto hutakiwa kuongezewa damu mara kwa mara.

Kutokana na upungufu huo wa damu, mtoto anakuwa katika maumivu makali sana, ndani ya siku 120 au miezi mitatu na kwamba dalili zake zinaanza kujitokeza sababu ya mwili kukosa damu baadhi ya maeneo.

Daktari anasema mfumo wa damu mwilini pia hupata hitilafu na kusababisha athari nyingine nyingi na athari hizo ni pamoja na ubongo kukosa damu na hatimaye.

Chanzo: habarileo.co.tz