Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Igembensabo mashuhuda wa kukuza uchumi kupitia  Ushirika Afya

003db8956074924df4d682ace061122e Igembensabo mashuhuda wa kukuza uchumi kupitia  Ushirika Afya

Wed, 19 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Igembensabo kilichopo wilayani Igunga Mkoa wa Tabora, ndio mnufaika wa kwanza wa Mpango wa Ushirika Afya unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na taasisi za fedha (benki).

Mpango huo ulioanza kutekelezwa Septemba 2020 sasa umeshika kasi katika vyama vya ushirika vilivyo katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Tabora, Geita, Simiyu, Mwanza, Tanga na Mara.

Hadi kufikia Machi mwaka huu, zaidi ya wanachama 5,800 wamesajili na kunuifaika, na lengo kwa mujibu wa NHIF, ni kufikia wakulima zaidi ya 570,000 ifikapo Desemba mwaka huu.

Mpango huu ni sehemu ya mikakati inayotekelezwa na NHIF katika kuongeza wigo wa wananchi katika mfumo wa bima ya afya kama serikali inavyodhamiria. Kwa kuanzia mpango huu umeanza kujumuisha wakulima kupitia vya vyama vya ushirika vya mazao ya kimkakati kama vile pamba, chai, kahawa, tumbaku, korosho na mengineyo.

Kupitia mpango huu, benki mbali ya kuwakopesha wakulima pembejeo za kilimo na mitaji, zinaunga mkono juhudi za serikali katika kupanua wigo wa wananchi katika mfumo wa bima ya afya kwa kutoa mkopo wa bima ya afya usio na riba kwa wakulima, ambao hurejesha mkopo huo kwa kukatwa fedha baada ya kuuza mazao yao.

Kwa sasa wanachama wa Igembensabo wanafurahia matunda ya ushirikiano huo wa NHIF ambao kwa Igunga na Nzega wameungana na Benki ya Posta Tanzania (TPB) katika kuwafikia wakulima hao, na hivi karibuni wameongeza ushirikiano na Benki ya CRDB ambayo inatarajiwa kuwafikia wakulima zaidi ya 300,000 katika mpango huo wa Ushirika Afya.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Igembensabo, Lazaro Ngulo anakiri kuwa mpango huo umewasaidia sana wanachama wake. Cha hicho kinaundwa na vyama vya ushirika wa mazao 56.

Katika mahojiano na gazeti hili, Ngulo anaeleza kuwa mchakato wa kuanzishwa kwa Ushirika Afya kwao ulianza Machi mwaka jana kwa mradi wa majaribio katika Chama cha Jilela Balimi Mwamashimba kilichopo Kata ya Mwisi.

“Mwanzoni tulifanya vikao na watu wa bima ya afya, maofisa wa TPB na wa ushirika, kisha tulifanya mkutano mkubwa pale Dodoma na tukaanza kuja kuwahamasisha wenzetu hapa (Igunga),” alieleza Ngulo na kukiri kuwa mwanzo ulikuwa mgumu kutokana na dhana ya bima ya afya kwa baadhi yao kutoeleweka vizuri.

“Lakini baadaye mambo yalienda vizuri na sasa hivi kuna mwitikio mkubwa wa wanachama wetu kujiunga katika ushirika huu ambo unawahakikishia kupata matibabu. Tuliona ushuhuda pale Mwisi siku ya uzinduzi mwezi Septemba baada ya mmoja wa viongozi kupata ajali ya bodaboda akija katika uzinduzi. Lakini kwa kuwa kadi yake ilikuwa tayari, alipelekwa katika Hospitali ya Malolo akapata matibabu yote, tunamshukuru Mungu hivi sasa amepona,” anasema mwenyekiti huyo.

Kauli yake inaungwa mkono na viongozi kadhaa wa vyama vya ushirika wa mazao vinavyounda Igembensabo ambao wanakiri kuna mwitikio mkubwa wa wanachama kujiunga na bima ya afya kupitia Ushirika Afya umekuja baada ya kuona wenzao waliojiunga mapema kunufaika na huduma za NHIF.

Katibu wa Chama cha Jilela Balimi cha Mwamashimba, Yegela Vasinel anaeleza kuwa tayari wanachama wake 128 kati ya 236 wamejiunga na mpango huo, na sasa kumekuwa na mwitikio mkubwa wa waliobaki kutaka kujiunga na huduma hiyo, na hivyo kwa sasa wanashughulikia taratibu za kujiunga na chama kwanza.

“Mwitikio ni mkubwa sana, mwanzo watu waliamini ni propaganda tu, hakuna huduma zozote. Lakini baada ya kushuhudia uzinduzi, kupata elimu na kuona wenzao wamefaidika na huduma hizi, watu wanakuja kwa wingi kutaka nao waingizwe katika mpango huu,” anaeleza Vasinel.

Anaongeza, “Tumewaambia wasubiri kwa sababu lazima kwanza uwe mwanachama wa ushirika ndio tuweze kukiingiza katika huduma ya bima… sasa hili haliwezekani hadi tuitishe mkutano wa chama ambao utabariki kwanza wawe wanachama na ndipo tuwaombee na huduma ya bima ya afya kama wenzao.”

Mkutano wa wanachama wa Jilela Balimi ulitarajiwa kufanyika Aprili 29, mwaka huu ambao ungeridhia kuwaingiza wanachama wapya pamoja na kusimamia utekelezaji wa kupata kadi za bima.

Katibu wa Chama cha Igunga Balimi, Adelina Braz ni shuhuda mwingine wa jinsi alivyopata huduma siku chache tu baada ya kujiunga na Ushirika Afya, hatua iliyosaidia sana na familia yake katika kupata matibabu.

“Mimi niliumwa siku chache baada ya kupata kadi, nikaenda katika hospitali ya wilaya nikiwa na wasiwasi na kadi yangu… Nilipofika na kuiwasilisha dirishani, ilionekana ni halali na nikapewa fomu, nikaenda kumwona daktari na kupatiwa matibabu,” anaeleza Braz ambaye chama chake kina wanachama 227 na wanufaika wa bima zaidi ya 98.

Anaongeza, “Niliporudi tu, nikawaonesha wengine ile fomu ya bluu tunayorudi nayo nyumbani… Nikawaambia hili jambo ni la kweli, mimi nimetibiwa bila shida yoyote, huu ni mpango wa kweli, sio ujanja ujanja.”

Anafafanua kutokana na bima, anasema hivi sasa amewakatia wategemezi wake wanne Bima ya Afya na anaoona kuwa kiwango cha Sh 76,800 wanachokatwa na benki, ni nafuu na kupitia Ushirika Afya, wameokoa fedha nyingi kwani awali walikuwa wanatibiwa katika hospitali binafsi kwa gharama kubwa zaidi.

“Nilienda hospitali binafsi mwaka 2019, nilikuwa nimelazwa nikalazimika kutumia zaidi ya shilingi 900,000, kwa sababu sikuwa na bima. Huu ushirika umekuja kutuokoa sana, sikutegemea kama ipo siku ningekwenda hospitali bila ya fedha na kuonesha kadi na kutibiwa, tena bila kubagua huduma,” alisema kiongozi huyo wa Igunga Balimi Amcos.

Anamtaja Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kuwa kutetea Watanzania wote kupata bima ya afya, akisema serikali imeleta mpango mzuri, hivyo anomba uendelee kusimamiwa vizuri kwani unawapunguzia mzigo mkubwa wa gharama wananchi ambao wengi hawana uwezo wa kumudu gharama kubwa za matibabu.

“Lakini sasa unaweza kutibiwa kwa shilingi 76,800 tu kwa mtu mzima au shilingi 50,400 kwa mtoto. Kwa kweli mimi nawahamasisha wenzangu kwamba wajiunge na mpango huu kwa kuwa unatusaidia sisi wakulima ambao sio wakati wote tuna fedha, kwani wakati mwingine tunakosa fedha sababu hatujavuna mazao,” anabainisha Braz.

Kiongozi mwingine wa Chama cha Nguzujise Amcos, Mussa Kindija anasema kupitia ushirika huo wenye wanachama 18, tayari wanachama 12 wamejiunga na bima ya afya, na wameona matunda yake kwa muda mfupi.

Anawashukuru viongozi wao wa Igembensabo kwa kuona umuhimu wa kujiunga na Ushirika Afya kwani inasaidia wanufaika wengi kwa sababu hata usipokuwa na fedha, bima inakuwezesha kupata matibabu wakati wote.

Kwa upande wake, Katibu wa Itogelo Balimi, Boniface Katagu anasema bima ya afya imekuwa mwokozi kwa wakulima wao kwa sababu mpango huo wa NHIF na benki umewarahisishia kupata matibabu, na jukumu lao ni kuendeleza kilimo kwa sababu wana uhakika wa matibabu wakati wote.

“Huu ni kama upendeleo kwa wakulima kwa sababu bado kuna watu wengi hawana bima za afya, lakini sisi wakulima wa Igunga kupitia chama chetu cha Igembensabo tumefikiwa na tunafaidi huduma hii, ni jambo kubwa kwetu, mwanzo tuliona kama tunadanganywa wakati walipoanza kutueleza,” anasema Katagu.

Akiwasilisha bungeni bajeti yake wiki iliyopita Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima alisema katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021, NHIF ilikuwa na lengo la kusajili wanachama wapya 413,368.

“Mfuko ulifanikiwa kusajili wanachama wapya 418,972 sawa na asilimia 101 ya lengo ikilinganishwa na wanachama 338,236 mwaka 2019/20. Katika kipindi husika, mfuko ulikuwa na wanachama 1,127,956 na wanufaika 4,341,993 sawa na asilimia 8 ya Watanzania wote ikilinganishwa na wanachama 1,050,493 na wanufaika 4,102,144 mwaka 2019/20,” alisema Dk Gwajima.

Amesema katika mwaka wa fedha 2021/22, NIHF imepanga kuongeza wigo wa wanachama kwa kutekeleza mkakati wa masoko na kubuni na kuanzisha vifurushi vya bima ya afya ikiwemo kifurushi cha wageni wanaoingia nchini.

Ni kwa kupitia mpango kama huu wa Ushirika Afya, nia ya serikli ya kuhakikisha Watanzania wote wanakuwa na bima ya afya itafikiwa kwa haraka na kuwa na taifa lenye watu wenye uhakika wa matibabu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz