Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Idadi ya watoto wanaozaliwa na maambukizi ya Ukimwi yapungua nchini

Idadi Ya Watoto Wanaozaliwa Na Maambukizi Ya Ukimwi Yapungua Nchini Idadi ya watoto wanaozaliwa na maambukizi ya Ukimwi yapungua nchini

Tue, 15 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI – The U.S. President’s Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR) ukitimiza miaka 20 tangu uanzishwe mnamo mwaka 2003, mafanikio makubwa yameelezwa kufikiwa nchini Tanzania ikiwemo watoto wengi kuzaliwa bila Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI lakini pia maambukizi kupungua kufuatia wanaume kupata huduma ya tohara kinga.

Akizungumza Jumatatu Agosti 14,2023 na Waandishi wa Habari wanaofanya ziara Mkoani Mara kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 20 ya PEPFAR, Mratibu wa PEPFAR nchini Tanzania Bi. Jessica Greene amesema mapambano dhidi ya UKIMWI yamekuwa na matokeo chanya kwa kupunguza maambukizi hususani kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

“Tunapotimiza miaka 20 ya PEPFAR nchini Tanzania tunajivunia kuwa na matokeo chanya kwa watoto. Wakati tunaanza mpango wa PEPFAR ,kwa watoto wengi walikuwa wanaambukizwa Virusi vya UKIMWI kupitia mama zao wenye maambukizi ya VVU, na sasa hii ni dunia tofauti maana kuna watoto wengi wanaozaliwa bila kuwa na maambukizi kutokana na huduma ambazo mama zao wanazipata kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua”,amesema Greene.

“Sasa hivi watoto wengi wanaishi maisha wakiwa wenye afya njema na tunaelekea kwenye kizazi kisichokuwa na maambukizi ya UKIMWI ,haya ni mafanikio makubwa sana tuliyofikia tangu Serikali ya Marekani na Serikali ya Tanzania ilianzisha Mpango wa PEPFAR mnamo mwaka 2003 baada ya Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush kutangaza Mpango wa Dharura wa Kukabiliana na UKIMWI”,ameeleza Bi. Greene.

Amefafanua kuwa PEPFAR kupitia Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (The U.S. Center for Disease Control -CDC) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau mbalimbali wakiwemo Amref Health Africa Tanzania wamekuwa wakitekeleza afua mbalimbali za afya kama vile kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto lakini pia kutoa bure huduma ya tohara ya kitabibu kwa wanaume. “Serikali ya Marekani ndiyo mfadhili mkubwa zaidi wa misaada ya VVU/UKIMWI nchini Tanzania, ikiwa imewekeza zaidi ya dola bilioni 6.6 kumaliza janga la VVU. Tuna ubia na makampuni ya madawa na wabia wenye wigo mkubwa wa usambazaji ili kukuza upatikanaji wa ARV. PEPFAR inafadhiliwa moja kwa moja kutoka serikali ya Marekani kisha ufadhili huo unapelekwa kwa mashirika watendaji manne nchini Tanzania ambavyo ni USAID, Kituo cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa CDC, Walter Reed, Idara ya Ulinzi na Peace Corp.Tumejitahidi kutanua kazi zetu kwenye vituo vya afya”,ameongeza Bi. Greene.

“PEPFAR ilipoanza kazi nchini Tanzania, kulikuwa na watu wasiozidi 1,000 waliokuwa kwenye matibabu. Leo PEPFAR inasaidia zaidi ya watu milioni 1.5 kwenye matibabu ya ARV ya kuokoa maisha. Mwisho wa VVU/UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo 2030 ni lengo kubwa linaloweza kufikiwa”,amesema Bi. Greene.

Amesema Serikali ya Marekani inajivunia kushirikiana na Serikali ya Tanzania kufikia malengo ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Kupambana na Ukimwi Duniani (UNAIDS) 95/95/95 (95% ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao, 95% ya waliogundulika wako kwenye matibabu, 95% ya wanaopata matibabu virusi vitakuwa vimefubazwa ifikapo 2025.

Mkurugenzi Mkazi wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC) nchini Tanzania Bw. Mahesh Swamination.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (The U.S. Center for Disease Control -CDC) nchini Tanzania Bw. Mahesh Swamination amesema huduma za tohara kinga wanazozitoa bure kwa wavulana na wanaume Mkoani Mara ili kuzuia maambukizi ya VVU kwa asilimia 60 zimesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi ya VVU kwenye migodi na makambi ya Wavuvi.

“Tumekuwa tukitoa huduma za tohara kinga bure kwa wanaume kwenye vituo vya afya lakini kwa kuwafuata wananchi kwenye maeneo yao kupitia huduma ya Mkoba ambapo huwa tunapeleka huduma ya tohara katika jamii mfano kwenye migodi na makambi ya wavuvi. Huduma ya tohara inafanya vizuri Mara licha ya changamoto ya mila”,ameeleza bw. Swamination.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha afya Murangi kilichopo katika halmashauri ya Musoma, Dkt. Anceth Elias amesema kituo hicho kimekuwa kikitoa huduma za tohara kwa wanaume ikiwemo kupeleka huduma za tohara kwa wavuvi na wachimbaji wa madini ambapo mwitikio ni mzuri kwani tangu walipoanzisha huduma ya tohara kinga bure mwaka 2018 wanaume 35,539 wamepatiwa huduma ya tohara na wameendelea kujitokeza kupata huduma

Chanzo: www.tanzaniaweb.live