Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili, imetoa idadi ya wagonjwa wa akili wanaopokelewa kwa siku ambayo inazidi idadi ya madaktari bingwa waliopo katika hospitali hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dkt. Paul Lawala amesema hospitali hiyo imekuwa ikipokea wastani wa wagonjwa 70 wa Nje (OPD), kwa siku wa afya ya akili huku ikiwa na madaktari bingwa 4 wa huduma hiyo.
Amesema, kwa sasa hospitali hiyo inahudumia wagonjwa 400 waliolazwa kutokana na matatizo ya afya ya akili, wagonjwa 500 ni warahibu wa dawa za kulevya pamoja na wagonjwa 250 wanaohudumiwa kisheria kutoka gereza kuu la Isanga.
Dkt. Paul amesema, kutokana na kuongezeka kwa matukio ya kikatili na mauaji kwenye jamii, yanadhihirisha kukua kwa tatizo la akili ambayo husababishwa na sababu mbalimbali na idadi hiyo haiendani na uwiano wa watoa huduma waliopo pamoja na Vifaa Tiba hivyo ameiomba Serikali kuendelea kuchochea uwekezaji katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Daktari wa vyanzo vya akili Veronica Lyimo amesema asilimia kubwa ya wagonjwa wanaofika hospitalini hapo hukutwa na sababu za kibaiolojia, saikolojia na kijamii.
Maadhimisho ya wiki ya afya ya akili ni Oktoba 7-10, 2022 jijini Dodoma ambapo huduma ya kupima afya ya akili, uzito, shinikizo la damu, kupata elimu ya afya ya akili, elimu ya saikolojia na athari za madawa ya kulevya zitatolewa.