Wataalamu waonya huenda kukazuka aina mpya ya kirusi cha Corona katika wakati huu ambao China inashuhudia kiwango kikubwa cha maambukizi katika mwezi huu, na hivi karibuni ikiondoa masharti ya kuthibiti kuenea kwa Uviko.
Wakati onyo hilo likitolewa baadhi ya mataifa ikiwemo Marekani yametangaza masharti mapya kwa wasafiri kutoka China.
Katika wiki tatu za kwanza za mwezi Desemba pekee, inakadiriwa watu milioni 248 nchini China waliambukizwa virusi hivyo.
Huku hospitali na sehemu za kuchomea maiti zikielemewa,katika taifa hilo ambalo hivi karibuni mamlaka ilitangaza kusitisha sera yake ya udhibiti wa maambukizi iliokuwepo tangu kuzuka kwa janga hilo miaka mitatu iliopita.
Wataalamu wa masuala ya afya wanahofia kwamba China itakuwa ni kitovu cha kuzalisha aina mpya ya virusi, ambapo hadi sasa vinaweza kusambaa miongoni mwa karibu moja ya tano ya watu duniani ambao hawana kinga ya kutosha na wale ambao hawajachanjwa.