Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huduma za kibingwa zinavyofungua milango ya wagonjwa kuja Tanzania

Ce1a97b604fa04ee60d33f54c463a3f1 Huduma za kibingwa zinavyofungua milango ya wagonjwa kuja Tanzania

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

IJUMAA iliyopita tulianza kuangalia namna uwekezaji mkubwa unaofanyika kwenye sekta ya tiba Tanzania, hatua ambayo inaonesha muda si mrefu Tanzania itakuwa kitovu cha utalii wa matibabu Afrika.

Tuliangalia namna kanda zote nchini zilivyosheheni hospitali za Kanda zinazotoa tiba murua zikiwemo za kibingwa na ukweli kwamba sasa hivi huduma nyingi za tiba ambazo tulikuwa tunazifuata nje ya nchi zinapatikana hapa hapa Tanzania.

Hali kadhalika tuliona kwamba, mbali na hospotali hizi kuwa na vifaa vya kisasa, pia zina watalaamu wa kitanzania wanaotoa huduma za kibingwa.

Uwepo kwa maabara na mashine zingine za uchunguzi nchini kumefanya huduma za kibingwa kusogezwa karibu na wananchi hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa wakisafiri kwenda nje ya nchi kufuata huduma za matibabu.

Huduma hizi za kibingwa zimepunguza idadi kubwa ya wagonjwa waliokuwa wanasafiri au kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu kwa zaidi ya asilimia 95 kutokana na uboreshaji wa huduma za afya ndani ya nchi.

Kwa sasa huduma kama hizi za uchunguzi kama CT Scan, MRI na maabara za kisasa zinapatikana katika hospitali zote kubwa za Kikanda za Serikali, Binafsi na za Mashirika ya dini.

Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) haikuachwa nyuma katika mapinduzi ya sekta ya afya nchini ambapo serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 9.5 kununua mashine mbili za kisasa za uchunguzi na tiba ya saratani.

Hatua hii imesaidia kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri tiba ya mionzi kutoka wiki sita hadi wiki moja.

Halikadhalika, Serikali imeweza kuokoa takribani Sh bilioni 10.4 kila mwaka za kuwasafirisha wagonjwa kutibiwa nje ya nchi. Elewa kwamba mgonjwa mmoja wa matibabua ya saratani anapokuwa nje ya nchi hugharimu kati ya Sh milioni 50 hadi Sh milioni 75.

Mashine zilizoletwa ORCI ni aina ya Linear Accelerator (LINAC) zinazotumia teknolojia ya 3D kutambua saratani kwa haraka katika mwili wa binadamu.

Februari 11 mwaka huu, taasisi hiyo ilipata mashine ya kisasa ya saratani inayotumia teknolojia ya juu na ya kisasa zaidi ambayo ni njia ya mawimbi na sauti inayokwenda kuongeza ufanisi na uharaka wa huduma.

Nataka kuzungumza kwamba uwepo wa vifaa hivi vya kisasa na vya kitaalamu vinaifanya Tanzania kuwa na faida ya ushindani (competitive advantage) dhidi ya nchi zingine barani Afrika, hivyo itasaidia sana kufungua wigo mpana kwa wagonjwa wengi wa nje ya nchi kuja na kupata huduma bora zaidi.

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kama mhimili mkuu wa afya nchini imekuwa na mafanikio makubwa sana katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano kwani kuna mambo mengi ambayo yalikuwa ni historia kufanyika nchini lakini leo imekuwa ni kitu cha kawaida.

Mwezi Novemba, 2017 Muhimbili iliingia kwenye historia baada ya kufanya upandikizaji wa figo wa kwanza nchini uliofanywa na madaktari bingwa kutoka hapo Muhimbili wakishirikiana na wataalamu wa afya kutoka hospitali ya BLK ya nchini India ambapo wagonjwa wote walifanyiwa upasuaji na kuwekewa figo mpya.

Takwimu zinaonesha kwamba upandikizaji wa figo unagharimu Sh milioni 21 ikiwa mgonjwa atapata matibabu hayo ndani ya nchi lakini nje ya nchi gharama huwa kati ya Sh milioni 80-100 kwa mgonjwa.

Kinachofurahisha ni kwamba upandikizaji wa figo haufanyiki Muhimbili pekee bali pia katika Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dodoma.

Kingine ni upandikizaji wa uroto (bone marrow transplant) unaotarajiwa kuanza hivi karibunu.

Muhimbili pia inafanya vizuri katika matibabu ya matibabu ya mfumo wa juu na kati wa chakula (Gastroenterology) ambapo kwa sasa ni kituo cha mafunzo, utafiti, uchunguzi na tiba katika Afrika Mashariki na Kati kwa matibabu hayo.

Mafanikio hayo yamesaidia kupunguza fedha ambazo serikali ilikuwa inatumia kuwatibu wagonjwa nje ya nchi.

Uwepo wa hospitali pamoja na vituo vingine vya ngazi mbalimbali za kutolea huduma za afya kama kliniki za madaktari bingwa (specialized clinics) na maabara za kufanyia uchunguzi (diagnostic centres) ambazo tayari zimeshapewa vyeti vya ithibati za kimataifa ni moja ya fursa kubwa kwa vituo hivyo kujitangaza na kuvutia mataifa mengi kuja kuhudumiwa Tanzania.

Hospitali na kliniki hizo zinapotambulika kimataifa maana yake ni kwamba vituo hivyo vinakuwa vimekidhi vigezo sawa sawa na vituo vingine vilivyo katika nchi zilizoendelea.

Kuna vituo vingi nchini ambavyo tayari vilishakidhi ubora na kupewa vyeti vya ithibati ikiwemo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).

Vituo vingie ni Hospitali ya Aga Khan (AKH), Regency Medical Centre, Lancert Laboratories, Smiles Dental Clinics, TMJ Super-Specialized Clinic, Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC), Saifee Hospital, Sali Internation Hospital pamoja na vituo vingine vingi nchini.

Ukichukua mfano wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete utaona kwamba taasisi hii imekuwa ikipokea wagonjwa wengi sana wa ndani na nje ya nchi wanaokuja kupata matibabu na uchunguzi wa kitaalamu wa moyo kama kuziba matundu, upasuaji wa kufungua moyo, kuzibua mishipa ya damu na kuweka kifaa maalumu cha kusaidia kurekebisha mapigo ya moyo ili yawe sawa (cardiac pacemaker) bila kusahau matibabu mengine mengi ya moyo.

Uwekezaji huu mkubwa wa serikali katika ujenzi wa taasisi za namna hii, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya tiba na uchunguzi pamoja na kusomesha wataalamu wengi zaidi wa afya kumepelekea kupunguza kwa zaidi ya asilimia 95 ya rufaa za nje ya nchi katika magonjwa ya moyo, figo, saratani, mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.

Hatua hii imeokoa mabilioni ya fedha ambazo zilipaswa kwenda nje ya nchi na hivyo kusaidia kuwa sehemu ya kuimarisha fedha zetu za kigeni.

Kwa sasa JKCI inapokea wagonjwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Msumbiji, Malawi, Zambia, Comoro n.k.

Tumeona pia mabalozi wengi wanaowakilisha nchi mbalimbali wakitembelea taasisi ya JKCI na kuisifu kwa utoaji wa huduma bora na za uhakika. Kwa mfano, Januari 28, 2019 Naibu Balozi wa Ujerumani baada ya kutembelea taasisi hiyo alisema anafurahishwa sana na hatua kubwa zinazopigwa kwenye suala la matibabu ya matatizo ya moyo yanayofanywa katika taasisi hiyo.

Mwandishi wa mkala haya ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ni msomaji wa gazeti hili.

Chanzo: www.habarileo.co.tz