Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huduma za afya, uzazi wa mpango bado tatizo Simiyu

13277 Pic+afya TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi, mkoa wa Simiyu ulioanzishwa Machi 2012 una jumla ya wakazi milioni 1.4 na pengine kutokana na kasi yao ya kuzaliana hivi sasa wanaweza kuwa wengi zaidi.

Katika mkoa huo wenye wanawake wengi kwa asilimia 52 zaidi ya wanaume, asilimia 54 ya watu wake ni watoto (walio chini ya miaka 18) na asilimia moja tu ndiyo wamevuka miaka 80.

Ripoti ya uwezo ya mwaka 2015 inaonyesha kati ya watoto wenye umri wa miaka tisa hadi 13 kati yao asilimia 63 tu ndiyo wanaojiunga na shule na baadaye asilimia 5 kati yao huacha kusoma kwa sababu mbalimbali.

Mkoa huo wenye wilaya tano kwa asilimia kubwa wakazi wake ni wasukuma na shughuli zao za kiuchumi ni ufugaji, kilimo na uvuvi kwa asilimia ndogo wilayani Busega, wilaya ambayo imepakana na Ziwa Victoria.

Watu wa Simiyu wanapenda kufuga ng’ombe wengi, kumiliki ardhi kubwa na hata kuwa na watoto wengi kwao ni ufahari, kuna kisa cha shule moja ya msingi mkoani humo ambayo wanafunzi wake wote wanazaliwa na wanaume 10 pekee.

Angela George, ofisa maendeleo ya jamii kata ya Somanda wilayani Bariadi anasema kuna kesi za wanawake kupigwa kwa sababu ya kutaka kutumia njia za uzazi wa mpango lakini pia hata wanawake nao wapo wenye kasumba ambao wanaamini kuwa watazaa mpaka ukomo wa uwezo wao wa kuzaa.

“Uzuri na ubaya wa watu wa Bariadi ukienda kuwahamasisha kuhusu jambo fulani wanakupokea kwa shangwe kubwa lakini utekelezaji ni hafifu hususani wanaume,” anasema George.

Mzee Mabula Mayara (79) mkazi wa Bariadi vijijini anasema hakumbuki idadi halisi ya watoto wake lakini ni wengi wengine walifariki na hata mtoto wake wa mwisho tayari naye ana familia yake.

“Wakati wetu sisi tulikuwa tunazaa watoto wengi na tulikuwa na uwezo kuwatunza lakini kwa sasa si rahisi watu wengi wakiwemo watoto wangu wanaishia kuzaa watoto kumi au tisa, wasukuma wana mbegu nyingi. Hata mimi bado ninazo,” anasema.

Suzan Marulu mkazi wa Busega anasema kuzaa watoto wengi ni muhimu na Mungu ameagiza hivyo kwa sababu wakati mwingine unaweza ukaacha kuzaa kumbe ungeendelea ungepata mtoto wa kukusaidia baadaye.

“Mimi nina watoto tisa, wanasaidia katika kilimo lakini kama ni wa kike akiolewa mapema ndiyo vizuri na yeye akajenge mji wake na analeta mahari, wa kwanza posa yake ilikuwa ng’ombe 11 na wa pili ng’ombe saba,” anasema Marulu. Anasema huduma za uzazi wa mpango ni za kilaghai kwani mtu akitumia anaweza kukaa hata miaka mitano bila kupata ujauzito jambo linalosababisha watu kuzaa uzeeni. “Bora ukazaa ukamaliza tu mayai mapema, ukifikisha watoto 15 yanaanza kuisha.”

Jinsi huduma za afya zilivyo

Hata hivyo licha ya watu wa Simiyu kupenda kuwa na watoto wengi lakini huduma za afya hususan ya mama na mtoto bado duni.

Naibu katibu mkuu, Ofisi ya Rais, Tamisemi, anayehusika na masuala ya afya, Dk Zainab Chaula anasema, Simiyu ina vituo vya afya 13 ambavyo bado si vingi lakini vitano tu ndivyo vinatoa huduma za dharura na upasuaji lakini hata hivyo si kwa ubora unaotarajiwa.

“Asilimia 80 ya wanawake wote ndiyo wanaojifungua kawaida 20 inaweza kutokea shida ndiyo maana tunahamasisha vituo vyote viwe na huduma ya dharura ili inapotokea jambo lolote iwe rahisi kwake kupata huduma kwa wakati,” anasema Dk Chaula.

Anasema inapozungumziwa huduma bora kwa hospitali za wilaya ni pale mgonjwa anapoweza kupata huduma za dharura, upasuaji mdogo, huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na uwepo wa vipimo tofauti.

Hata hivyo anasema Serikali inaendelea kuhamasisha kina mama wote waende kliniki ili wapatiwe elimu ya matunzo tangu ujauzito hadi kujifungua sanjari na kufanya jitihada za kuboresha huduma.

Sally Shaku ni daktari mfawidhi hospitali ya wilaya Meatu mkoani Simiyu, anasema katika wilaya hiyo wajawazito hulazimika kusubiriana hata kama wapo katika hali ya kutaka kujifungua kutokana na changamoto ya ufinyu wa wodi ya kujifungua na miundombinu kwa ujumla.

Anasema miundombinu ya chumba cha upasuaji ilikuwa finyu na hata wodi ya wazazi ilikuwa ya kubanana, uwezo wake ulikuwa wagonjwa 10-16 kwa siku lakini wanaojifungua kwa siku ni 12-19.

“Chumba maalumu cha kujifungulia katika wodi ya wazazi licha ya kuwa wanaohitaji kujifungua ni 12-19 lakini kilikuwa kinatosha kuhudumia mtu mmoja mmoja hivyo wengine walikuwa wanasubiri wodini, huko wanakaa na ambao hawajaanza kupata uchungu,” anasema.

Anasema kutokana na hali hiyo wakati mwingine mama anajifungua akiwa bado yupo sehemu ya kusubiria kwa sababu ya wingi wa wazazi na uchache wa vyumba vya kujifungulia na upungufu wa wataalamu, “Hapa nina wastani wa wataalamu 127 lakini walitakiwa wawepo 300.”

“Hatari kubwa iliyopo si tu mtu kupoteza maisha akijifungulia wodini lakini pia ni rahisi kwa mama na mtoto kupata bakteria,’’ anasema Dk Shaku.

Hata hivyo Dk Shaku anasema pamoja na tatizo hilo lakini jambo la kujivunia ni kwamba wataalamu na wadau mbalimbali wamefanya jitihada kupunguza vifo vya kina mama na watoto 19 kwa mwaka hadi vifo viwili.

Hata hivyo anasema kuna tatizo la uelewa wa wananchi wilayani Meatu kwani uhudhuriaji kliniki si mzuri na hata wanaokuja wanakuja kwa kuchelewa.

Mjamzito ajifungua kwenye foleni

Yulita Elikadi aliwahi kumshuhudia mjamzito akijifungua akiwa kwenye foleni akisubiri huduma ya kitabibu katika kituo cha afya cha Nasa, wilayani Busega.

Elikadi ana miaka (42 na ana watoto tisa walio hai anaishi kijiji cha Mwamsikule B, Busega, watoto wake wengine wanne walifariki kwa sababu mbalimbali. “Ni miaka sita iliyopita nilimsaidia mama mmoja alijifungua mtoto wa kiume, unaweza kuona ni muda mrefu umepita lakini sijasahau tukio hilo ni historia katika maisha yangu,” anasema.

Anasema mwaka 2012 alifika kituo cha afya cha Nasa, ilikuwa saa nne asubuhi na alipofika aliungana na wazazi wengine waliokuwa wakisubiri huduma ya kliniki ndipo mmoja wao akashikwa na uchungu wa uzazi ghafla.

Anasema mama huyo alianza kupiga yowe na watu walianza kukimbia lakini yeye alimuonea huruma baada ya kuona mtoto alianza kutoka hivyo alimfuata ili kumpa msaada wa mapema kwa kuwa wakunga wakati huo walikuwa wako ‘bize’ wanawasaidia wazazi wengine.

“Mimi ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kwenda kliniki, vizazi vitano kabla nilijifungulia nyumbani hivyo nilifanya kukumbuka tu jinsi wakunga wa jadi walivyokuwa wakinihudumia, sikuwa na kifaa chochote zaidi ya kanga lakini nilimsaidia yule mama akajifungua salama,” anasema Elikadi.

Anasema baada ya mtoto kuzaliwa alikuwa hana kifaa cha kukata kitovu lakini baada ya muda nesi alikuja na kumsaidia.

Hivi karibuni Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Korea (Koika) limekuwa likitekeleza mradi wa ‘Nilinde nikulinde’ mkoani Simiyu unaolenga kufanya maboresho ya huduma za uzazi na vyumba vya upasuaji katika vituo vya afya.

Mradi huo unajumuisha uboreshaji vituo 12 kati 38 vilivyopo, kupitia mradi huo magari tisa mapya aina ya Toyota Land Cruiser yalikabidhiwa kwa ajili ya kubebea wagonjwa na shughuli za uratibu mkoani humo. Thamani ya mradi mzima hadi kukamilika ni Sh5.52 bilioni.

Katika uzinduzi wa vituo hivyo mwakilishi mkazi wa UNFPA Tanzania, Jackline Mahon alisema lengo la mradi ni kuwawezesha wanawake na vijana katika afya kwa kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo endelevu na hata mipango ya Serikali.

Mwakilishi wa Koika, Kila Thomas anasema Koika iliona umuhimu wa kuokoa maisha ya wanawake na watoto wakati wa kujifungua “Tunaamini mwanamke hatakiwi kupoteza maisha wakati akitoa uhai kwa mtu mwingine”.

Meneja mradi wa afya ya Mama na Mtoto wa UNFPA, Felister Bwana, anasema kutokana na changamoto ya ubora wa huduma za afya ya mama na mtoto zinazotolewa mkoani humo, shirika liliona umuhimu wa kusaidia kuimarisha sekta hiyo muhimu.

Anasema hospitali ambazo zimeboreshwa zimefungiwa mashine mbalimbali za uchunguzi na matibabu, vyumba vya upasuaji na wodi za wazazi zimewekewa miundombinu yote muhimu inayoruhusu wanawake wanne kujifungua kwa wakati mmoja.

Jambo jingine kubwa, lenye kufurahisha na kuibua matumaini ni kwamba katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga Sh105 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya za wilaya 67, kwa sasa hospitali za wilaya zipo 77.

Chanzo: mwananchi.co.tz