Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huduma za TB zasogezwa kwa wananchi

14519 PIC+TB TanzaniaWeb

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya ugatuaji kwa kusogeza karibu na wananchi huduma ya Kifua Kikuu (TB) sugu ili kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu.

Hayo yamesemwa leo Agosti 29 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa hospitali ya magonjwa ambukizi Kibong’oto kwa kamati ya huduma za jamii ya Bunge.

Ugatuaji huo utafanyika katika ngazi ya vituo vya afya 78 nchini.

Waziri Ummy amesema wamefanya ugatuaji  wa vituo hivyo vya afya ili kuwezesha wagonjwa kupata tiba jirani na jamii inayowazunguka na hivyo  kujenga uelewa wa wananchi juu ya ugonjwa na kushiriki kikamilifu katika kumhudumia mgonjwa hasa katika chakula, masuala ya kijamii na kisaikolojia.

Ameitaja mikoa ambayo vituo hivyo vipo ni pamoja na Kagera, Mtwara, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Mbeya, Pwani, Mrorgoro, Njombe, Iringa, Tanga, Mwanza,  Lindi na Pemba na kuongeza kuwa hadi sasa wagonjwa wapatao 112 wamepata huduma  za tiba ya TB sugu.

Hata hivyo mnamo mwaka 2017 Serikali kwa kushirikiana na mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) ilizindua kituo bora katika hospitali hiyo kwa kutoa huduma za afya kwa wachimbaji wa migodi wanaougua magonjwa ya TB, mapafu na usikivu unaosababishwa na ulipuaji baruti migodini.

Tangu kuanzishwa kituo hicho wagonjwa 863 wamepata huduma, wagonjwa 614 walipima makohozi na 116 (asilimia 19) waligundulika kuwana TB na 123 (asilimia 15) walikuwa na magonjwa ya mapafu yanayosababishwa na vumbi na 125 (asilimia 15.3) walikuwa na upotevu wa usikivu.

Chanzo: mwananchi.co.tz