Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali ya mkoa Njombe kuanza huduma Julai 2019

51543 Pic+njombe

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Njombe umekamilika kwa asilimia 96 na ifikapo Julai mwaka huu hospitali hiyo itaanza kutoa huduma.

Ummy ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 10, 2019 katika mkutano wa hadhara unaofanyika katika viwanja vya Sabasaba mjini Njombe ikiwa ni sehemu ya ziara ya Rais John Magufuli mkoani humo.

Ummy amesema ifikapo Julai 2019 Serikali itairejesha hospitali teule ya Kibena kwa halmashauri ya Njombe ili wananchi waendelee kupata huduma.

“Tumejipanga kipindi cha miezi miwili kuweka vifaa na vifaatiba na kusimika mashine mbalimbali za kutolea tiba, tunao watumishi 149 ambao tutawapanga katika hospitali hii utakayoweka jiwe la msingi leo, hospitali hii itakuwa na madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali wakiwemo mabingwa wa magonjwa ya watoto, wajawazito na kinamama, mionzi na magonjwa ya ajali, mifupa, na mengineyo,” amesema Ummy Mwalimu.

Aidha Ummy amesema hivi sasa jumla ya madaktari bingwa 311 wanasomeshwa na mfuko wa Serikali uliotenga Sh2.5 bilioni kwa ajili ya ufadhili huo na wamewapa mikataba kwamba ni lazima watumikie serikalini angalau kwa miaka mitatu kabla ya kuamua kwenda sehemu nyingine.

“Rais umetupatia Sh3.5 bilioni na ndani ya mwezi mmoja tunaanza kujenga wodi ya kulaza wagonjwa, wagonjwa wa ndani, upasuaji wa mifupa na ndani ya mwaka mmoja majengo yote yatakamilika na tumepata fedha Sh3 bilioni kutoka Global Fund,” amesema Ummy.

Aidha amesema Serikali ina lengo la kujenga nyumba 10 za watumishi katika kufanikisha hospitali hiyo kutoa huduma za rufaa karibu na wananchi hawa.

“Tumeleta karibu huduma za uchunguzi wa CT Scan na magonjwa mengine, sasa hamtakwenda Mbeya bali mtapewa huduma hapahapa, Fedha za dawa mkoa ulipewa Sh456milioni kwa mwaka 2015 na sasa fedha zinazotengwa ni Sh1.4 bilioni, kwa halmashauri ya Njombe ilitengwa Sh44 milioni sasa ni Sh177 milioni,” amesema Ummy.



Chanzo: mwananchi.co.tz