Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali ya Sekou-Toure kupewa mashine ya CT-Scan

11352 Hos+pic TanzaniaWeb

Sat, 14 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Serikali imeahidi kutoa mashine ya CT-Scan katika Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.

Pia, imeahidi kutoa Sh1.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za mama na mtoto ili kukabiliana na vifo vitokanavyo na uzazi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo alipotembelea hospitali hiyo juzi na kuongeza kuwa Serikali inataka wodi ya mama na mtoto katika hospitali hiyo kuwa na hadhi ya juu.

“Moja ya vipaumbele vyetu ni kuboresha maeneo ya mama na mtoto. Serikali inataka kuboresha huduma hizo, tumeamua kuiangalia hospitali hii kwa namna ya kipekee kwa sababu inahudumia watu wengi na fedha hizi zikitumika vizuri tumepanga tutaongeza nyingine lengo ni kuondoa changamoto hizi,” alisema Waziri Mwalimu.

Awali, akitoa taarifa kwa waziri, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Bahati Msaki alisema wameshatumia Sh350 milioni kwa ajili ya kukarabati wodi ya mama na mtoto.

Pia, alisema licha ya hospitali hiyo kuhudumia wagonjwa wengi, lakini haina mashine ya CT-Scan.

“Hatuna daktari bingwa wa usingizi, mifupa na daktari bingwa wa mkoa kwa magonjwa ya upasuaji, hivyo tunapata changamoto katika huduma hizo,” alisema Msaki.

Chanzo: mwananchi.co.tz