Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kuanza kusafisha damu

Tumbi Picv  V Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kuanza kusafisha damu

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: mwanachidigital

Wakati Serikali ikiweka mkazo katika huduma za kusafisha damu (dialysis), hospitali ya Rufaa ya Tumbi mkoani Pwani, inatarajiwa kuanza kutoa huduma hiyo Desemba 15, 2022.

Hatua hiyo itapunguza adha ya rufaa kwa wagonjwa wanaohitaji huduma ya dialysis katika hospitali hiyo ambapo kwa wiki watu watatu hadi watano hupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Hata hivyo, utolewaji wa huduma hiyo katika hospitali ya Tumbi utaongeza idadi ya hospitali za rufaa zitakazokuwa na mitambo ya kuchuja damu kutoka mikoa saba au zaidi.

Akizungumza ofisini kwake jana, Desemba 5, 2022, mtaalamu wa magonjwa ya ndani katika Hospitali ya Tumbi, Dk Adam Gembe amesema mitambo tisa imefungwa na Bohari ya Dawa (MSD) ili kufanikisha kazi hiyo.

“Tunaishukuru MSD kwa kutuletea mitambo hii ya kuchuja damu, kufikia katikati ya mwezi huu (Desemba) tunatarajia kuanza kutoa huduma ya kuchuja damu,” amesema.

Kutolewa kwa huduma hiyo, amesema kutawapunguzia wagonjwa wa figo na sukari katika mkoa huo, safari ya kufuata huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Kwa wiki tulikuwa tunatoa rufaa za wagonjwa kati ya watatu hadi wanne kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kupatiwa huduma ya dialysis, tunaamini tunavyoanza kutoa hapa tutawapunguzia gharama pia,” ameeleza.

Pamoja na MSD kufunga mitambo hiyo, Dk Gembe amesisitiza kuharakisha upatikanaji wa vitendanishi ili huduma hizo zitakapoanza kutolewa zisikwame.

Kilango Mchala ni mfamasia katika hospitali hiyo, ameeleza kwamba licha ya juhudi za usambazaji wa dawa zinazofanywa na MSD, zinahitajika bidii zaidi kufanikisha upatikanaji utakaotosheleza.

“Kwa sasa tunashukuru wametupa utaratibu wa haraka wa kupata dawa kwa kutumia maduka yao ya nje, unaandika mahitaji yako, wanaangalia kilichopo wanakukamilishia,” amesema Mchala.

Mfamasia wa MSD, Kanda ya Dar es Salaam, Diana Kimario amezitaka hospitali kutoa taarifa ya mahitaji ya dawa na vifaa tiba kabla havijaisha kabisa.

“Hospitali zikae kufanya tathmini ya matumizi yao ya mwaka na walete MSD, hiyo itarahisisha usambazaji, sio kesho zinakwisha leo ndio unaleta mahitaji,” ameeleza mfamasia huyo.

Chanzo: mwanachidigital