Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali ya Rufaa Chato kuanza kuchuja, kusafisha damu

Chato Pic Hospitali ya Rufaa ya Chato

Thu, 4 Aug 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato itaanza kutoa huduma ya kuchuja na kusafisha damu baada ya kupata mashine 10 za kutoa huduma hiyo.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Osward Yapa alisema mashine hizo zimenunuliwa na Serikali kwa nia ya kusogeza huduma karibu na wananchi wanaotibiwa hospitalini hao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa hafla ya kuzindua huduma ya bure kwa wagonjwa wenye matatizo ya moyo, kisukari, upumuaji, magonjwa ya wanawake na watoto, Dk Yapa alisema kazi ya kufunga mashine hizo inatarajiwa kukamilika mwezi huu.

Kwa sasa, huduma ya kuchuja na kusafisha damu inapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza, inayohudumia wagonjwa kutoka mikoa minane ya Kanda ya Ziwa na Ziwa Magharibi, ikiwamo Mwanza, Kigoma, Tabora, Geita, Kagera, Mara, Simiyu na Shinyanga.

“Kupatikana kwa mashine hizi ni ukombozi kwa wagonjwa ambao awali walilazimika kufuata huduma Bugando jijini Mwanza,” alisema Dk Yapa.

Tangu ifunguliwe mwaka jana, Hospitali ya Rufaa Chato yenye vitanda 83 imehudumia wagonjwa zaidi ya 10,000 waliofanyiwa uchunguzi na kupata huduma za kibingwa za matibabu ambao awali walilazimika kufuata huduma Bugando jijini Mwanza.

Advertisement “Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 201. Ujenzi utakapokamilika katika awamu zote, hospitali yetu itakuwa na vitanda 800, huku wagonjwa kati ya 7,000 hadi 10,000 wakitarajiwa kuhudumiwa kwa mwaka,” alisema.

Dk Yapa alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali hiyo iliyoanza mwaka 2017 ikihusisha majengo manne imekamilika na iligharimu zaidi ya Sh16.72 bilioni, huku awamu ya pili inayohusisha jengo la mionzi, wodi yenye vitanda 201, hewa tiba na maegesho ya magari itagharimu zaidi ya Sh18.5 bilioni na tayari Serikali imetoa zaidi ya Sh9 bilioni.

Akizungumzia rasilimali watu, Dk Yapa alisema hospitali hiyo yenye watumishi 227 kwa sasa inatarajiwa kuwa na idadi ya watumishi 1,154 wa idara na vitengo mbalimbali.

Changamoto

Pamoja na mafanikio, hospitali hiyo bado inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kukosekana kwa magari maalumu kwa ajili ya shughuli za kiutawala, kusafirisha wagonjwa, kukusanya damu, majengo kwa ajili ya kufulia nguo, kuhifadhi maiti, kutakasa vifaa yiba, upasuaji na jengo la mama na mtoto.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz