Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali ya Muhimbili yasogeza huduma zake mikoani

21299 Muhimbili+pic TanzaniaWeb

Mon, 8 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanzisha programu mpya ya kuzijengea uwezo hospitali zote za rufaa ijulikanayo kama Mkoba.

Programu hiyo italenga zaidi maeneo yenye upungufu wa wataalamu au yenye wataalamu lakini wanahitaji kuongezewa ujuzi zaidi katika fani mbalimbali.

Akizungumza leo Jumapili Oktoba 7, 2018 na waandishi wa habari, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa MNH, Aminael Aligaesha amesema  programu hiyo ambayo ni endelevu itahusika na kuwajengea uwezo wataalamu katika hospitali zote za rufaa nchini.

"Programu hii ni sehemu ya mpango mkakati wa hospitali iliyojiwekea kuhakikisha inatembelea hospitali za rufaa za mikoa yote nchini ili kushirikiana nao katika kutoa huduma kwa wananchi ambao wangepewa rufaa kuja Muhimbili kupata matibabu wakati huohuo tukiwajengea uwezo wataalamu wa hospitali hizo," amesema.

Aligaesha amesema katika kutekeleza programu hiyo kwa mara ya kwanza jana imepeleka jopo la wataalamu 14 katika Hospitali ya Rufaa Musoma mkoani Mara.

"Hii ni programu endelevu ambayo itakuwa inafanya kazi ya kutembelea hospitali nne kila baada ya robo mwaka na kwa mara ya kwanza jana tumepeleka wataalamu Hospitali ya Rufaa Musoma, watafanya kazi kwa siku tano." amesema.

Amesema wataalamu hao watakuwa na kazi ya kutoa huduma na kuwajengea uwezo wataalamu katika hospitali hizo katika huduma za upasuaji wa watoto, watu wazima  na akina mama.

Amesema kutakuwa na  upasuaji wa njia ya mkojo, huduma za macho, upasuaji wa pua koo na masikio.

Aligaesha ameongeza wataalamu hao pia watakuwa wanatoa huduma ya tiba ya dawa ya usingizi na patholojia.

"Tunatoa wito kwa wananchi walioko Musoma na Mara wajitokeze kwa wingi ili wanufaike na huduma hizo na utaratibu wa kupata huduma hizo  ni uleule kama unaopatikana Muhimbili" amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz