Dodoma. Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imesema Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila ina upungufu wa watumishi kwa asilimia 50.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Februari 6, 2020 na mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo bungeni mjini Dodoma.
Amesema tangu kuanzishwa kwake kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa ndani na nje kwa asilimia 48, na wagonjwa wa upasuaji kwa asilimia 107 pamoja na ongezeko la makusanyo ya mapato.
Amesema pamoja na mafanikio hayo, baadhi ya changamoto hizo ni upungufu huo wa watumishi, ukosefu wa nyumba za watumishi, uhaba wa wataalam wa kutumia vifaa vya kisasa jambo linaloathiri utendaji bora.
“Hospitali zenye vigezo hivyo (kama Mloganzila) zimekuwa zikitumika kutoa huduma za kibingwa na kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi kwenda kupata huduma na kuchangia kuongeza pato la Taifa na nchi kujulikana duniani,” amesema.
Amesema kamati hiyo inashauri hospitali hiyo itumike kutoa huduma za kibingwa ili kuvutia wagonjwa wa ndani na nje ya nchi na kuwa sehemu ya utalii wa matibabu.
Pia Soma
- Serikali ya Tanzania yaagiza tani 225,000 za mbolea
- Rais Magufuli ayashukia mabaraza ya ardhi
- Askofu Maboya asema watafunga siku saba kuwaombea waliokufa kongamano wa Mwaposa
Amebainisha kuwa hilo likifanyika itasaidia kuongeza pato la Taifa na nchi kujulikana duniani kama ilivyo India.