Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali ya JKCI yafanya upasuaji wa mishipa ya damu bila kusimamisha moyo

F03a2241f9ab3d4772e9cbb0eb5e5753.jpeg Hospitali ya JKCI yafanya upasuaji wa mishipa ya damu bila kusimamisha moyo

Thu, 4 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KWA mara ya kwanza madaktari wazawa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wamefanya upasuaji wa kihistoria kwa kupandikiza mishipa ya damu bila kusimamisha moyo.

Mkuu wa Idara ya Upasuaji katika taasisi hiyo, Dk Evarist Nyawawa alilieleza gazeti hili kuwa, upasuaji kama huo ulikuwa ukifanyika kwa ushirikiano na madaktari wa nje tofauti na sasa ambapo wamefanya wazawa pekee.

Alisema walianza upasuaji huo Oktoba 28 mwaka huu kwa kupandikiza mishipa kwa wagonjwa watatu.

Dk Nyawawa alisema jopo la madaktari wanane walifanya upasuaji huo kwa kati ya saa nne hadi nne na nusu na akabainisha kuwa muda huo ni mfupi kulinganisha na upasuaji unaofanywa kwa kusimamisha moyo.

Alisema miongoni mwa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji huo, mmoja alikuwa na tatizo la kuziba mishipa miwili hivyo uwezo wa moyo kufanya kazi ulishuka na kubaki asilimia 27.

Dk Nyawawa alisema wagonjwa wawili walikuwa na tatizo na kuziba mshipa mmoja na mara nyingi wamekuwa wakifanya upasuaji wa aina hiyo kwa kusimamisha moyo.

“Wakati wa kumpandikizia yule ambaye ana shida ya mishipa miwili ilitupa shida kidogo kwani mshipa mmoja uko ndani ya moyo baada ya kufungua kifua hivyo tulifanya bila kuathiri moyo,” alisema.

Alisema JKCI ina idadi ya kutosha ya madaktari wenye uwezo wa kufanya upasuaji wa kibingwa na pia wana vifaa vya kisasa.

“Kutokana na teknolojia na vifaa tulivyonavyo tunaendelea kuwagundua na kuhudumia wagonjwa wengi hivyo tuna ongezeko kubwa la wagonjwa wanaofika hospitali sasa,” alisema Dk Nyawawa.

Mmoja wa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji huo, John Ticky alisema alipata tatizo la shinikizo la damu lililosababisha kuziba kwa mishipa baada ya kuumwa ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz