Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali ya JKCI kupokea madaktari bingwa kutoka China

Ce86a9840221efeaa33455a135cdc936 Hopsitali ya JKCI kupokea madaktari bingwa kutoka China

Mon, 13 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI za Tanzania na China zimesaini mkataba wa ushirikiano katika sekta ya afya kwa lengo la kuleta madaktari bingwa na uboreshaji wa miundombinu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Ushirikiano huo upo tangu mwaka 1968 lakini ulisitishwa kwa muda kutokana na mlipuko wa virusi vya corona ulioanza mwishoni mwa mwaka 2019.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa utiaji saini mkataba huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Doroth Gwajima alisema umekuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania.

"Kumekuwa na utamaduni wa kuhuisha mikataba ya ushirikiano, serikali ya Tanzania imenufaika na mambo mengi kutokana na ushirikiano huu hasa suala la kupokea madaktari kutoka China wa fani mbalimbali za kibingwa.”

"Hadi sasa zaidi ya wataalamu 1,000 kutoka China wamefika nchini na kuhudumia hospitali mbalimbali ikiwamo Tabora, Dodoma, Mara na kwingineko, lakini pia tumekuwa tukipokea dawa na vifaa tiba vingine kutoka nchini humo tangu tuanze ushirikiano huu," alisema Dk Gwajima.

Alisema taasisi ya JKCI ambayo imehudumia maelfu ya Watanzania na wageni ni matokeo ya ushirikiano huo.

"Karibu watu 300,000 wameshapata huduma wakiwamo 800 ambao wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa wazi na watu zaidi ya 2,000 wamepata huduma ya umeme wa moyo,” alisema Dk Gwajima.

Alisema ushirikiano huo pia umehusisha tafiti zikiwamo za dawa asili na watu wengi wamenufaika na pia wataalamu wamekwenda China kupata uzoefu.

"China inatusaidia kupanua Hospitali ya JKCI iweze kubeba wagonjwa wengi na tunataka kupeleka kule Mloganzila majengo yapanuliwe zaidi,” alisema.

Aidha, alisema serikali inaendelea kuwasilisha maombi mengi ikiwamo upanuzi wa huduma katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na huduma nyingine za kibingwa ziendelee kutazamwa katika ushirikiano huo.

"Vilevile huduma ya tiba asilia pia tumeweka katika ushirikiano huu na wizara imetenga eneo la ekari 1,000 Kisarawe ili kuotesha miti kwa ajili ya kufanya utafiti wa dawa maana wao wako juu katika suala hili,” alisema.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Abel Makubi alisema mkataba huo una manufaa makubwa kwa wananchi katika eneo la tiba asilia.

Chanzo: www.habarileo.co.tz