Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali ya JKCI imefanya upasuaji wa kubadili mshipa mkuu wa damu

Ce527cd34220dbc1838e0a16b8e9e6b0 Hospitali ya JKCI imefanya upasuaji wa kubadili mshipa mkuu wa damu

Thu, 11 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Madaktari Bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wazawa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanya upasuaji wa kubadilisha mshipa mkubwa wa damu (Aorta) uliokuwa umetanuka pamoja na valvu yake (Aortic valve insufficiency) bila ya usimamizi wa madaktari kutoka nje.

Mafanikio hayo yanakuja baada ya miaka kadhaa ya kujifunza upasuaji huo kutoka kwa wataalam wenzao wanaofika JKCI kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.

Upasuaji huo unaojulikana kama Bentall Surgery uliochukua saa tano kukamilika. Ulifanyika hivi karibuni ambapo mgonjwa anaendelea vizuri na anatarajia kuruhusiwa wakati wowote kuanzia sasa.

Mgonjwa huyo alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya kifua na baada ya uchunguzi aligundulika kuwa mshipa mkubwa wa damu (aorta) unaotoa damu kutoka kwenye moyo na kusambaza damu mwili mzima.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk Godwin Sharau amesema tatizo hilo mara nyingi huwapata watu wengi wenye umri wa kuanzia miaka ya 50.

Amesema mara kadhaa huwapata watu wanaosumbuliwa na shinikizo la damu la muda mrefu hivyo mshipa huo kupoteza umahiri wake wa kuweza kustahimili presha.

Dk. Sharau ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto amesema kwa mgonjwa ambaye hatapata matibabu husika kwa wakati mshipa huo huendelea kutanuka na hivyo kupelekea kufa ghafla.

“Kwa miaka mingi upasuaji wa Bental operation kwa hapa JKCI umekuwa ukifanyika lakini chini ya usimamizi wa madaktari wenzetu kutoka nje ya nchi, sasa wataalam wetu wameonesha umahiri mkubwa wa kufanya upasuaji huu. Hii ni hatua nzuri sana katika Taasisi yetu”, alisema Dk. Sharau.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live