Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali ya Benjamin Mkapa kufanya upasuaji wa mdomo sungura bure

17000 Pic+mdomo+sungura TanzaniaWeb

Fri, 14 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) itaanza kutoa huduma ya upasuaji wa midomo sungura au midomo wazi  bila malipo.

Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Septemba 12,  Makamu Mkuu wa Chuo cha Udom, Profesa Egid Mubofu amesema kuwa huduma hiyo itaanza kutolewa hivi karibuni katika Hospitali ya Benjamini Mkapa na kuwataka wananchi wote wenye matatizo hayo kujitokeza kwa wingi.

“Hivi karibuni hospitali yetu ya Benjamini Mkapa itaanza kutoa huduma ya upasuaji wa midomo sungura au midomo wazi, huduma hiyo itatolewa bure kabisa kwa hiyo watu wote wenye matatizo hayo wajitokeze kwa wingi kutibiwa,” amesema Profesa Mubofu.

Amesema tarehe rasmi ya kuanza kutoa huduma hiyo itatangazwa hivi karibuni.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dk, Alphonce Chatanda amesema kuwa Hospitali hiyo itaendelea kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi  kwani serikali imewekeza gharama kubwa kwenye vifaa tiba, wataalamu na dawa ili kuwawezesha Watanzania wengi kupata huduma hapa nchini.

Amesema kuwa wananchui wengi  wametibiwa magonjwa waliyotakiwa kutibiwa nje ya nchi kwa gharama nafuu na kupona kabisa ambapo hivi sasa wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji mali.

“Serikali inaposema kuwa inakwenda kwenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda haiwezi kufanikiwa bila kuwekeza kwenye sekta ya afya kwa sababu nguvu kazi kubwa ya uchumi huo ni wananchi ambao wanatakiwa kuwa na afya njema,” amesema Dk, Alphonce Chatanda.

Hadi sasa Hospitali ya Benjamini Mkapa imeshafanya huduma ya

kupandikiza figo kwa wagonjwa wanne ambapo mwezi Machi mwaka huu walimfanyia mtu mmoja na Agosti mwaka huu wamewafanyia wagonjwa watatu ambao wote wameruhusiwa kutoka hospitalini kuendela na majukumu yao.

Chanzo: mwananchi.co.tz