Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Tiba na Afya wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Ahmed Jusabani amesema moto uliowaka katika jengo la duka la dawa ni mdogo na haujaleta athari yoyote.
Dk Jusaban ameyasema hayo leo Oktoba 28, 2019 katika viunga vya hospitali hiyo Jijini Dar es Salaam, Tanzania huku akisisitiza kuwa moto huo uliwaka katika jengo la dawa za wagonjwa wa nje na walipotoa taarifa, jeshi la zima moto walifika kwa haraka na kufanikiwa kuuzima moto huo.
Amesema sehemu iliyoathirika ni ndogo na kwa sasa wanaendelea kufanya usafi katika eneo hilo.
“Sababu ya moto huu bado hatujajua na hatujajua vitu gani vimeungua tutatoa taarifa baadaye. Hakuna aliyeathirika na ndugu wenye wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Aga Khan wasiwe na wasiwasi na wagonjwa wa nje watatumia duka la dawa la wagonjwa wa ndani,” amesema Dk Jusaban.
Naye mgonjwa Rukia Hassan aliyekwenda kutibiwa hospitalini hapo amesema akiwa ndani anasubiri kupatiwa matibabu ghafla aliona moshi ukitokea eneo hilo ndipo akakimbia na kutoka nje ya jengo hilo.
“Nipo nje tumeambiwa tusubiri tusiingie ndani tutaitwa baadaye, kwa kweli ule moshi niliokuwa nimeuona niliogopa,” amesema Rukia.