Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali nyingine ya saratani kujengwa Dar

Saratani Agizo Hospitali nyingine ya saratani kujengwa Dar

Sat, 19 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hospitali ya saratani inatarajiwa kujengwa Dar es Salaam chini ya mradi mtambuka wa saratani (TCCP) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa na Aga Khan Foundation.

Meneja wa mradi huo kutoka Aga Khan Foundation, Dk Harrison Chuwa alisema jana kuwa hospitali hiyo itakayohudumia asilimia 35 ya wagonjwa wa msamaha na asilimia 65 wa kulipia na bima, ujenzi wake utaanza mwezi ujao.

Chuwa alisema hayo kwenye semina iliyoandaliwa na taasisi hiyo kwa waandishi wa habari kwa lengo la kuwaelimisha juu ya utoaji wa habari za afya na zaidi kuhusu ugonjwa wa saratani.

Akizungumzia mipango mbalimbali ya mradi huo wa saratani unaotekelezwa katika mikoa mwili nchini, Chuwa alisema miongoni mwake ni ujenzi wa hospitali hiyo ya saratani itakayojengwa Dar es Salaam karibu na Hospitali ya Aga Khan.

Kujengwa kwa hospitali hiyo itakayomilikiwa na Aga Khan ambayo ndiyo yenye andiko la kwanza kuhusu mradi, kutafanya nchi kuwa na taasisi nyingine kubwa ya huduma hiyo baada ya Ocean Road.

Kwa mujibu wa mwakilishi huyo wa AKF, tayari wameshapata vibali vyote kutoka Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kwamba jiwe la msingi litawekwa mwezi ujao. Alisema ujenzi utachukua miezi 18 na matarajio ni kwamba ifikapo Desemba mwakani, mgonjwa wa kwanza ataanza kutibiwa.

Kwa mujibu wa Dk Chuwa, hospitali itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 150 kwa siku.

Hii ni kutokana na mashine mbili zitakazowekwa kila moja kuwa na uwezo wa kutibu wagonjwa 50. Akizungumzia mradi mtambuka wa saratani, alisema una thamani ya takribani Sh bilioni 39 huku Shirika la Maendeleo la Ufaransa likiwa limetoa Euro milioni 10 na AKF dola za Marekani milioni 3.3.

Mradi huu unaotekelezwa kwa miaka minne katika mikoa ya Dar es Salaam ambako unakwenda halmashauri zote nane na tano za Mkoa wa Mwanza, utasaidia vituo 100 vya afya vya serikali kuanzia zahanati hadi hospitali za mkoa.

Malengo ya mradi ni uboreshaji wa miundombinu na vifaa tiba vya huduma za saratani.

“Na katika hili, kwa kuwa mradi umeanza Januari 2020, umeshatoa mashine moja ya ultra sound ya kisasa yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 150 kwa taasisi ya Ocean Road kwa ajili ya kufanya vipimo ambavyo kipindi cha nyuma walikuwa hawawezi kufanya,” alisema Dk Chuwa. Alisema mashine hiyo iliyoanza tangu Februari mwaka jana, kwa sasa inahudumia watu takribani 50 hadi 80 kwa siku.

Kwa mujibu wa Dk Chuwa, mashine hiyo ya kisasa ni ya pili kwa Tanzania na ya tatu katika Afrika Mashariki.

Pia mradi una mpango wa kufunga mashine kwa ajili ya kutoa matibabu ya mionzi ya ndani katika koromeo la mlo katika Taasisi ya Saratani Ocean Road. Itakuwa ya kwanza kutolewa katika Afrika Mashariki na Kati.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live