Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali nyingine 3 zajiandaa kusafisha figo

E542f394942d533505e8da2c271fb65e Hospitali nyingine 3 zajiandaa kusafisha figo

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KITENGO cha magonjwa yasiyoambukiza katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kimesema hospitali tatu za rufaa za mikoa zinamalizia maandalizi ya kuanza kutoa huduma ya kusafisha figo.

Ofisa katika kitengo hicho, Dk Linda Ezekiel alisema jana Dar es Salaam kuwa, hadi mwaka 2009 hakukuwa na hospitali ya serikali iliyokuwa ikitoa huduma hiyo hadi sasa hospitali sita za rufaa zinasafisha figo.

“Ikaanza Muhimbili, ikaenda KCMC, Bugando, Benjamin (Mkapa), kwa hospitali za kanda tukawa tumemaliza, tumeanza sasa hizi hospitali za rufaa za mikoa, Bombo wameanza (Tanga) huduma kuanzia mwaka jana Februari, Mount Meru wameanza Januari saa hivi tuna hospitali sita” alisema.

Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya figo alisema, Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mtwara wamefunga mtambo na huenda ndani ya mwezi mmoja au miwili wataanza kutoa huduma hiyo.

‘Musoma iko tayari wakati wowote, walikuwa wanasubiri kifaa kimoja cha jenereta waweze kuanza huduma. Maweni wameshafunga mashine Kigoma, nao wako mbioni kuanza huduma ndani ya miezi miwili mitatu” alisema Dk Linda wakati akizungumza kwenye kipindi cha 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds kinachomilikiwa na kampuni ya Clouds Media ya Dar es Salaam.

“Ifikapo Juni Kigoma, Ligula, Sekouture, Kagera, Musoma, Bombo nimesema na Mount Meru hizo hospitali saba tutakuwa tumekamilisha. Na mpango ni kwamba, mikoa yote 26 ifikapo 2025 iwe yote inaweza kutoa huduma za usafishaji wa figo”alisema Dk Linda.

Daktari Bingwa wa Figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Francis Furia alisema gharama za kusafisha figo zinaanzia sh 180,000 hadi 300,000 kwa mara moja na kwamba, mgonjwa hutakiwa kufanyiwa huduma hiyo walau mara tatu kwa wiki.

Juzi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima alisema, takwimu zinaonesha kuwa, hapa nchini kuna wagonjwa sugu kati ya 4,800 hadi 5,200 wanaohitaji huduma ya kusafisha damu au kupandikizwa figo.

Dk Gwajima aliyasema hayo jijini Mbeya wakati akitoa tamko la serikali kuhusu maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani iliyoadhimishwa jana.

“Kati ya hao wagonjwa 1000 wanapata huduma ya usafishaji wa damu kwa sasa. Hadi kufikia Novemba 2020 jumla ya wagonjwa 316 wamepandikizwa figo katika hospitali mbalimbali” alisema.

Dk Gwajima alisema wagonjwa 78 wamepandikizwa figo nchini wakiwemo 62 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na 16 Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma.

Mwaka jana Dk Linda alilileza HabariLEO kuwa kupandikiza figo nchini kunagharimu sh milioni 30 na mgonjwa akienda kupata tiba hiyo nje ya nchi gharama huwa mara tatu zaidi.

Alisema chanzo kikuu cha magonjwa ya figo ni kisukari, shinikizo la juu la damu, homa ya ini, maambukizi ya virusi vya ukimwi, na maambukizi ya magonjwa ya bakteria hasa kwenye njia ya mkojo (UTI).

Chanzo: www.habarileo.co.tz