Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali inayojengwa tangu Waziri Ummy akiwa darasa la 1

Fri, 30 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Musoma. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali imepania kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Nyerere mkoani Mara iliyoanza kujengwa mwaka 1980 wakati waziri huyo akiwa darasa la kwanza.

Waziri alisema hayo wakati alipotembelea hospitali hiyo na kuelezea kutengwa kwa Sh3 bilioni ambazo zitatumika kukamilisha ujenzi wa jengo la mama na watoto hospitalini hapo.

Alisema kutokana na ukubwa wa hospitali hiyo, wameamua ujenzi wake ufanyike kwa awamu, hali ambayo alisema itasaidia kutoa huduma wakati ujenzi ukiendelea.

Waziri Ummy ambaye wakati jengo hilo linaanza kujengwa alikuwa na miaka saba na akisoma shule ya msingi Chanika, alisema mara baada ya jengo hilo la akina mama na watoto kukamilika, huduma zianze kutolewa mara moja.

Alisema hospitali hiyo itatumika kwa huduma za rufaa.

Pia alisema Serikali inatarajia kufungua kitengo cha matibabu ya kibingwa katika hospitali hiyo.

Aliagiza Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Mifupa (MOI) kuangalia namna wanavyoweza kutoa huduma katika hospitali hiyo.

Awali mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alimuomba waziri huyo kusaidia fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika eneo la hospitali ili kurahisisha utoaji wa huduma mara ujenzi utakapokamilika. Malima pia aliwashukia baadhi ya watumishi wa idara ya afya kwamba wanakwamisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia mkoani humo. Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo.

Malima alisema baadhi ya watumishi wamekuwa wakishirikiana na watuhumiwa hasa wa ubakaji kupotosha taarifa ya vipimo wakati wahanga wa ubakaji wanapokwenda kupimwa.

Alitoa mfano wa hospitali ya wilaya ya Tarime ambako mtoto wa miaka minne alikuwa akilawitiwa, lakini alipopelekwa hospitalini hapo majibu yalionyesha hajalawitiwa.

“Ilibidi huyu mtoto nimpeleke Bugando (Mwanza),” alisema Malima.

“Majibu yakaonyesha alikuwa analawitiwa. Ilinilazimu kuhamishia kesi huku Musoma ili niweze kufuatilia kwa ukaribu na hatimaye mtuhumiwa akahukumiwa miaka 30 jela.”

Malima pia alitoa mfano tena wa binti wa miaka 12 aliyebakwa hivi katibuni wilayani Rorya, lakini alipopelekwa kupimwa katika kituo cha afya cha Utegi ilionekana hajabakwa . Alisema mtoto huyo alipopelekwa Hospitali ya Shirati, majibu yalionyesha kuwa alibakwa. Akizungumzia hali hiyo, Waziri Ummy alisema tayari amepokea malalamiko kama hayo na kwamba matukio kama hayo ni kinyume cha maadili ya kazi na kuagiza kuwa yeyote atakayebainika, achukuliwe hatua za kisheria.



Chanzo: mwananchi.co.tz