Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali iliyoanza kujengwa mwaka 1980 yatengewa Sh3bilioni

29445 MALIMA+PIC TanzaniaWeb

Fri, 30 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Musoma. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Sh3bilioni zitatumika kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la mama na watoto katika hospitali ya rufaa ya Mwalimu Nyerere iliyopo Mkoa wa Mara.

Ummy ametaja kiasi hicho cha fedha leo Alhamisi Novemba 29, 2018 baada ya kutembelea hospitali hiyo inayoendelea kujengwa, kuagiza mara baada ya jengo hilo kukamilika huduma zianze kutolewa mara moja.

Amebainisha kuwa Serikali imedhamiria kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 1980, kwamba kutokana na ukubwa wake wameamua ujenzi huo kufanyika kwa awamu, hatua aliyodai itasaidia kutoa huduma wakati ujenzi ukiendelea.

Amebainisha kuwa hospitali hiyo itaanza kutumika kama hospitali ya rufaa ya mkoa mara ujenzi utakapokamilika, pia Serikali inatarajia kufungua kitengo cha matibabu ya kibingwa katika hospitali hiyo.

Amesema ataiagiza Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na Hospitali ya Mifupa (MOI) kufika katika hospitali hiyo kuangalia namna wanavyoweza kutoa huduma katika hospitali hiyo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mara,  Adam Malima alimuomba waziri huyo kusaidia fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika eneo la hospitali ili kurahisisha utoaji wa huduma mara ujenzi utakapokamilika.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz