Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali KCMC, Rufaa Mbeya kuwa Taasisi – Serikali

KCMC 343.png Hospitali KCMC, Rufaa Mbeya kuwa Taasisi – Serikali

Mon, 12 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali kupitia Wizara ya Afya ilitenga zaidi ya Bilioni 5.4 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya jengo la mama na mtoto META, Hospitali ya Rufaa ya kanda nyanda za juu Kusini – Mbeya na tayari kupitia MSD vimepelekwa kwa ajili ya usimikwaji, huku ikisema Hospitali za Rufaa za kanda-Mbeya, na KCMC zinakuwa taasisi jambo litalo ongezewa mgao wa uendeshaji na kuboresha huduma kwa wananchi.

Hayo yamesemwa hii leo Juni 12, 2023 na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu, Suma Ikenda Fyandomo katika Mkutano wa kumi na moja Bungeni jijini Dodoma.

Amesema, “katika mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya jengo la huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya META ya Mkoa wa Mbeya.”

Aidha ameongeza kuwa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya META limeanza kutumika na ufungaji wa vifaa tiba katika vitengo mbalimbali unaendelea na unatarajia kukamilika mapema Mwezi Julai 2023 ili wananchi wanaohitaji huduma za aina mbalimbali waendelee kunufaika na huduma hizo.

Dkt. Mollel amesema, Serikali imeendelea kuboresha huduma katika vituo vyote vya utoaji huduma ikiwemo hospitali ya kanda ya KCMC huku zaidi ya Shilingi 983,612,500 hutumika kila mwezi kwaajili ya kulipa stahiki na mishahara ya watumishi 905 waliopo katika hospitali hiyo.

“Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imepeleka kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya Dawa, vitendanishi na vifaa tiba ili kuwahudumia wananchi wanaofika kupata huduma katika hospitali ya KCMC, huku kiasi cha Shilingi bilioni 5.9 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya hospitali hiyo na shilingi milioni 263.6 kwa ajili ya uendeshaji,” amesema Naibu Waziri.

Hata hivyo ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetoa ufadhili wa masomo ya ubingwa bobezi kwa watumishi 15 wa kada za afya wa KCMC wanaosoma ndani na nje ya nchi na kwamba Wizara ya afya kwa kushirikiana na Wizara ya fedha na OR Utumishi zinaendelea na mchakato ili kuhakikisha hospitali za Rufaa za kanda-Mbeya, pamoja na KCMC zinakuwa taasisi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live