Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hospitali Dar, Dodoma zaweka mitambo ya oksijeni

7844f8eb022c55bd3c1d6a6fc3c9a881.jpeg Hospitali Dar, Dodoma zaweka mitambo ya oksijeni

Fri, 9 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KUSIMIKWA na kuanza kazi kwa mitambo ya kuzalisha oksijeni katika Hospitali ya Amana, Dar es Salaam na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, kumetajwa ni hatua muhimu ya serikali kukabiliana na maradhi yakiwemo mlipuko wa corona kwani mitambo hiyo inaweza kuzalisha gesi ya kuhudumia hata wagonjwa 350 kwa wakati mmoja.

Akizungumza na HabariLEO jana, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume alisema mtambo huo wa kuzalisha/kutengeneza oksijeni umesimikwa Amana na una uwezo wa kuhudumia wagonjwa 150 kwa wakati mmoja.

Akizungumzia wimbi la tatu la corona ambalo limeshaingia nchini na tayari mikoa minne ukiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na Arusha ina wagonjwa wa maradhi hayo, Dk Mfaume alisema wamejipanga kama mkoa kuendelea kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.

“Mkoa wa Dar es Salaam tumejipanga kudhibiti corona, ni kweli wimbi la tatu limeingia na tuna wagonjwa, lakini serikali imejipanga vizuri kuhakikisha tunakabiliana nao, cha msingi kikubwa ni wananchi kubadilisha tabia, kwa sababu bado wapo wasiotaka kuvaa barakoa,tunasisitiza wananchi wote chukueni tahadhari,” alisema Dk Mfaume.

Alisema katika kukabiliana na corona, Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza taasisi, mamlaka na viongozi kila mmoja kwenye eneo lake kuhakikisha wanachukua tahadhari na kuelimisha wananchi, sambamba na kada ya afya kusimamia na kujiandaa kwa vifaa tiba ili iwapo mlipuko huo utatokea waweze kukabiliana nao.

Katika kutekelea hilo, serikali ilitoa Sh milioni 600 kwa ajili ya mradi huo wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha gesi ya oksijeni Amana ili isaidie wagonjwa wenye mahitaji ya hewa hiyo wakiwemo pia waathirika wa corona.

Hivi karibuni, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichalwe alitembelea mradi huo na kusema hizo ni juhudi za srikali katika kuboresha huduma za tiba nchini na kwamba maboresho yataendelea nchi nzima.

Kuhusu mitambo hiyo ya kuzalisha oksijeni, Dk Sichalwe alisema una matoleo zaidi ya 89 yenye uwezo wa kuzalisha mitungi 200 ya Okisjeni kwa saa 24, jambo linaloipa hospitali uwezo wa kuhudumia wagonjwa 150 wahitaji wa gesi hiyo 150 kwa wakati mmoja kila siku.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Best Magomba aliliambia gazeti hili jana kuwa ni kweli mkoa huo una wagonjwa wa corona na kuwataka wananchi wote wachukue tahadhari kwa kuvaa barakoa na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya bila kupuuza.

“Dodoma tulishajiandaa hatukusubiri tupate wagonjwa wa corona, tulianza mapema maandalizi ya kukabiliana na wimbi la tatu la ugonjwa huu, katika hospitali yetu ya mkoa tumefunga mtambo wa kuzalisha oksijeni ambao una uwezo wa kuhudumia hadi wagonjwa 200 kwa siku, iwapi watatokea kuhitaji huduma hiyo,” alisema Dk Magomba.

Akizungumzia mtambo huo na jinsi mkoa huo ulivyojipanga na hadhari ya Covid-19, alisema hivi sasa oksijeni sio tatizo katika hospitali hiyo na kuwa katika kila kitanda kwenye wodi mgonjwa mwenye uhitaji wa gesi hiyo anaipata.

Alisema katika wimbi hili la tatu la corona nchini, wananchi hawana budi kuchukua tahadhari kwa kuvaa barakoa na kuendelea kufuata maelekezo ya wataalamu ikiwemo kuepuka msongamano, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi na tiririka.

“Kwa sasa tunajimudu wenyewe na kwa wagonjwa wanaohitaji oksijeni bado hali sio mbaya, na hata iwapo wagonjwa wa corona wataongezeka labda 200 na wote wakahitaji oksijeni, bado tuna uwezo wa kuwahudumia wote kwa mara moja kila mmoja akapata hiyo gesi,” alisema Dk Magomba.

Chanzo: www.habarileo.co.tz