Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku 24 tangu Serikali itangaze kuwapo kwa homa ya dengue nchini, watu 1,222 wamegundulika kuugua ugonjwa huo jijini Dar es Salaam, Tanga na Singida huku wawili wakifariki dunia.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Aprili 12 watu 307 waligundulika kuwa na homa hiyo.
Akizungumza jana, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema kasi ya kukua kwa ugonjwa huo imeongezeka, “mpaka sasa, takwimu tulizonazo, Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na wagonjwa 1,145, Tanga tumepata wagonjwa 76 na Singida tumepata mgonjwa mmoja, lakini pia kuna vifo viwili vimetokea.” Takwimu hizo ni zile zilizokusanywa kuanzia Januari Mosi hadi Ijumaa iliyopita katika hospitali za umma na binafsi nchini.
Kuhusu mikakati ya Serikali kudhibti ugonjwa huo, Dk Ndugulile alisema vitendanishi kwa ajili ya uchunguzi vimeshawasili nchini na pia wizara imeshaziagiza halmashauri kuhakikisha zinanunua viuatilifu na kupuliza katika maeneo yote yanayopaswa.
“Rais John Magufuli alishatoa maelekezo, kila halmashauri inatakiwa kutenga fedha kwa ajili ya kununua viuatilifu na kusambaza katika maeneo yote ili kuua mazalia ya mbu na wadudu wengine, tunachokifanya sasa ni kuhamasisha wananchi wenyewe kuchukua hatua ikiwamo kujikinga kwa kutoweka maji yaliyotuama ndani, kuondoa mazalia ya mbu na kufyeka nyasi,” alisema.
Aidha, imelezwa kuwa dawa zote zenye diclofenac si salama kwa mgonjwa mwenye homa ya dengue ambazo ni Ibuprofen, Brufen na Diclopar.
Habari zinazohusiana na hii
- Wizara ya Afya yatoa tahadhari uwapo wa dengue Tanzania
- VIDEO: Asimulia alivyotambua kuwa na homa ya dengue
- MAONI: Wananchi wachukue tahadhari homa ya dengue
Alisema mbu wa dengue aina za Aedes Egypti, Aedes Albokictus na Aedes Africans, huuma mchana.