Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Homa ya Mgunda ni hatari kwa makundi haya

Ummy Mwalimu Afya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Wed, 20 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imeweka bayana kuwa ugonjwa unaowatesa baadhi ya watu mkoani Lindi, unajulikana kwa jina la homa ya mgunda na kutaja makundi ya watu wanaoweza kuathirika zaidi na ugonjwa huo uliolishtua Taifa katika siku za karibuni.

Serikali ilifikia hatua hiyo baada ya upimaji wa sampuli za wagonjwa waliokuwa wakiugua ugonjwa huo ambao awali haukujulikana

Majibu hayo yamekuja ikiwa ni siku nne kupita tangu Serikali ilipokubali ombi la Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha kukinga na kudhibiti magonjwa (CDC) cha Marekani, kuongeza nguvu kwenye timu ya wataalamu kubaini ugonjwa huo.

Imeeleza kuwa makundi ya watu wanaofanya kazi za kilimo, mgodini, maji taka, machinjio, madaktari wa mifugo, watunza wanyama na wafanyakazi wanaotengeneza bidhaa za maziwa, wanaweza kuwa hatarini kupata maambukizo ya homa hiyo kutokana na kazi wazifanyazo.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wameeleza kuwa licha ya dalili za homa ya mgunda kufanana na zile za ugonjwa wa marburg, wamechambua tofauti ya magonjwa hayo mawili.Wakizungumza na Mwananchi jana kwa nyakati tofauti, wataalamu hao walisema magonjwa hayo yote mawili yanasababishwa na bakteria na virusi watokao kwa wanyama.

Hata hivyo, homa ya mgunda imetajwa kuwa husababishwa na bakteria aina ya ‘Leptospira interrogans’ ambao hupatikana kwenye mkojo wa panya na wanyama wafugwao wakiwamo mbwa na ng’ombe, huku Marburg ukisababishwa na virusi ambavyo mara nyingi hutoka kwa popo kwenda kwa binadamu.

Mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati alisema magonjwa hayo mawili yana vyanzo tofauti.

“Marburg inasababishwa na virusi vinavyofanana na vile vya ebola na mara nyingi mgonjwa hutokwa na damu sehemu nyingi za mwili na mtu ukivipata ndani ya siku mbili mpaka 21, unaanza kupata dalili kama za homa kali na damu kutoka kwenye matundu ya mwili,” alisema Dk Osati.

Alisema homa ya mgunda inasababishwa na bakteria ambao mara nyingi wanapatikana kwenye mikojo ya wanyama kama panya au wale wafugwao nyumbani wakiwamo ng’ombe na mbwa.

“Mara nyingi wanyama wakikojoa na ukakutana na ule mkojo wao ikiwa wana hao bakteria, inaweza kusababisha mtu akapata hiyo homa, tofauti na marburg ambayo inapatikana kwa aina fulani ya popo. Homa ya mgunda inapatikana zaidi kwa wanyama kama panya zaidi na wale wa nyumbani wanaofugwa,” alisema.

Waziri wa Afya

Jana akitoa tamko kuhusu ugonjwa huo baada ya kutembelea wilaya ya Ruangwa, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema ugonjwa huo ulikuwepo katika maeneo ya kitropiki ambayo ni yenye hali ya joto katika mabara ya Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Afrika, Asia na Australia.

Alisema wanyama aina za panya, kindi, mbweha, kulungu, swala na wanyamapori wengine wameripotiwa kupata maambukizo ya vimelea hivyo na kuwa chanzo cha maambukizo kwa binadamu.

Alisema mpaka kufikia Julai 17, 2022, jumla ya wagonjwa 20 na vifo vya watu watatu vimetolewa taarifa.

“Kwa sasa wagonjwa wawili pekee wenye dalili bado wamelazwa katika eneo lililotengwa kwa ajili ya matibabu. Vilevile, timu zimeendelea na ufuatiliaji wa watu waliotangamana na wagonjwa na mpaka sasa hakuna aliyeonyesha dalili za ugonjwa huu,” alisema Waziri Ummy.

Maambukizo na matibabu

Waziri Ummy alisema ugonjwa huo huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kupitia uchafuzi wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji kutoka katika mkojo wa wanyama wenye maambukizi.

Alisema mtu anaweza kupata ugonjwa huo kwa kugusa mkojo (au maji maji mengine ya mwili) kutoka kwa wanyama wenye maambukizo, kugusa maji, udongo, au chakula kilichochafuliwa na mkojo wa wanyama wenye maambukizi au kunywa maji yaliyochafuliwa na vimelea vya bakteria wa ugonjwa huo.

Kuhusu matibabu yake, ugonjwa huo unatibiwa na viua sumu (antibiotic) kama doxycycline au penicillin. Mgonjwa anapaswa kunywa dawa hizi mapema katika kipindi cha ugonjwa huo.

Dawa hizi zinapaswa kutumiwa pia na wale wenye dalili kali zaidi. Inaelezwa pia kuwa hatari ya homa hiyo inaweza kudhibitiwa mapema kwa watu kutoogelea au kuzama ndani ya maji ambayo yanaweza kuwa na mkojo wa wanyama, au kutowagusa wanyama walioambukizwa.

Nguo au viatu vya kujikinga vinapaswa kuvaliwa na wale walioathiriwa na maji au udongo uliochafuliwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live