Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi ndizo sababu za pacha kuungana

48453 Pic+pacha

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wanasayasi wamechambua mambo yanayosababisha wazazi kujifungua pacha walioungana, matukio ambayo yamekuwa yakiongezeka katika miaka ya karibuni.

Pia, wametaja sababu za kuzaliwa pacha walioungana, wakisema ni pamoja na yai lililorutubishwa na kugawanyika mara mbili kutotenganishwa vizuri.

Sambamba na hilo, mtandao wa kimataifa wa Verywell Family, umeeleza kuwa nusu ya watoto pacha duniani kote huzaliwa mapema, kabla ya wiki 36 na wengi wao huzaliwa mimba ikiwa na miezi minane.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, wanasayansi hao walisema kwa kawaida pacha wapo wa aina mbili.

Wanasema wapo wale ambao huundwa na mayai mawili au zaidi ambayo hurutubishwa kwa pamoja, lakini wapo ambao huundwa na mbegu za kiume zisizofanana.

Inaelezwa kuwa mbegu za aina hiyo pia hutunga watoto zaidi ya wawili na wale wa yai moja, hurutubishwa na kutoa pacha wanaofanana.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Nathanael Mtinangi alitoa ufafanuzi juu ya sababu za mama kujifungua pacha au watoto zaidi ya wawili.

Alisema kuna sababu kuu mbili, moja ni ya kurithi yaani mama kuwa na vinasaba vya pacha ambao mayai hupevuka kwa wakati mmoja kutoka pande zote mbili.

“Wapo wanawake ambao hutoa mayai mawili. Kwa kawaida kila mwezi hutakiwa kutoa yai moja, kushoto na mwezi ujao kulia, lakini ikiwa mama anatoa pande zote kama ilivyo kwa baadhi ya koo zinatoa kila pande au matatu na wakati mwingine mawili kila pande, matokeo yake watoto hujiumba kulingana na mayai yanayopevushwa,” alisema daktari huyo.

Dk Mtinangi alisema aina ya pili ni ya wanawake ambao mayai yao hupevushwa na kisha kugawanyika mara mbili, hivyo kama yai moja litashuka, atapata pacha wanaofanana ambao hukaa kwenye mfuko mmoja, “akishusha pande zote mbili mayai ambayo yatagawanyika mara mbili, atapata watoto wanne wanaofanana ambao walikaa wawili katika kila mfuko.”

Kwa nini huungana?

Daktari Bingwa wa Watoto kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Francis Furia alisema wanaoungana ni pacha wanaofanana ambao chanzo chao ni yai moja lilorutubishwa kisha kugawanyika mara mbili.

“Sasa ikitokea lile yai halikugawanyika vizuri au halikukamilika kwenye kugawanyika kwake, ndiyo hutokea hali ya watoto kuungana na mara nyingi huwa ambalo haligawanyiki hasa tumboni au kifuani,” alisema.

Dk Furia alisema kati ya watoto 50,000 wanaozaliwa duniani kote, hutokea pacha walioungana mara moja.

Alisema hadi sasa hakuna sababu inayoeleza kwa nini hutokea hivyo, lakini wanasayansi wamebaini kuwa yai linapogawanyika baada ya mimba kutungwa kama halijakamilika kati ya siku 10 hadi 13, ndiyo husababisha hali hiyo.

Daktari bingwa wa maradhi ya kina mama na uzazi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Colman Living alisema tatizo la pacha kuungana hutokea kijenetiki.

Alisema wakati wa yai kugawanyika kuna hatua ambazo wengine hutengana mapema na wapo wanaochelewa.

“Wanaochelewa kugawanyika ndiyo mara nyingi huungana na utafiti umebaini wengi wanaoungana ni wa kike.”

Wenye maumbile tofauti

Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto kutoka Muhimbili, Zaituni Bokhari alisema kutotibu ugonjwa wa malaria wakati wa ujauzito, matumizi ya vyakula na vinywaji visivyo salama hasa vyenye gesi na tindikali, ni moja ya sababu za kuzaa watoto wenye maumbile tofauti au pacha walioungana.

Hata hivyo, alisema hakuna sababu maalumu hadi sasa, lakini kuna vitu vinavyosababisha kujifungua mtoto ambaye si wa kawaida.



Chanzo: mwananchi.co.tz