Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hizi hapa sababu watoto kususa kunyonya

Kunyonyesha Breast Feeding Hizi hapa sababu watoto kususa kunyonya

Mon, 20 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati takwimu zikionyesha idadi kubwa ya watoto wanazidi kukataa kunyonya ziwa la mama kabla ya kutimiza miezi 24, ripoti imeanika kuwa asilimia 50 hukataa ziwa wakifikisha miezi mitano.

Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) wa mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibuni, inataja kuwa chuchu bandia inayotoa maziwa mengi kwa urahisi na mama kukaa mbali na mtoto kwa muda mrefu ni miongoni mwa sababu zinazochangia watoto wengi kususa ziwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mtoto anapokataa kunyonya mama hunyong’onyea na kupata mawazo mengi.

Hata hivyo wataalamu wamebainisha kitendo cha mtoto kususa kunyonya ni njia ya kumwambia mama kwamba kuna kitu hakipo sawa.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa watoto wawili kati ya 10 hawanyonyeshwi kabisa maziwa ya mama zao baada ya kuzaliwa katika mwezi wa kwanza.

Utafiti huo ambao hutolewa kila baada ya miaka mitano, inaonyesha idadi ya wanaoacha kunyonya huongezeka hadi watoto watatu kati ya 10 wanapofikisha mwezi wa pili.

Ripoti imeonyesha idadi hiyo huendelea kuongezeka zaidi hadi watoto watano mpaka sita kati ya kumi wanapofikisha miezi mitano.

Ripoti hiyo imebaini katika umri wa mwezi 0 hadi mmoja asilimia 81 hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kulingana na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Asilimia hupungua hadi 68 kwa miezi miwili hadi mitatu na hadi asilimia 45 kwa miezi minne hadi mitano.

Hata hivyo, ripoti inaonyesha matumaini kwani mtindo wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee miongoni mwa watoto walio chini ya miezi sita umeongezeka kadiri muda unavyopita, kutoka asilimia 26 mwaka 1991-92 hadi 64 mwaka 2022.

Mkazi wa Mbezi, Anastella Balozi alisema mtoto wake wa kwanza alikataa ziwa alipofikisha umri wa miezi sita bila yeye kujua sababu.

"Alianza kukataa ziwa la kulia, alipofikisha miezi sita akasusa la kushoto. Niliumia lakini mpaka leo huwa nahisi sababu nilikuwa namuacha muda mrefu sababu ya kazi." alisema

Jamila Omary mama wa watoto wawili, alisema mtoto wake wa kwanza alikataa kunyonya akiwa na miezi tisa na wa pili alisusa ziwa alipofikisha miezi saba, hata hivyo hajui sababu.

Madaktari washauri

Daktari bingwa wa watoto kutoka Hospitali ya Aga Khan, Rukhsar Osman Mussa alisema ni muhimu kumnyonyesha mtoto kwa wakati mara tu mama anapojifungua.

“Mama asimwage maziwa yake ya mwanzo yenye rangi ya njano kwani haya ni muhimu na humpatia mtoto kingamwili dhidi ya magonjwa mbalimbali na aanze ndani ya saa moja baada ya kujifungua kwani hii itasaidia kuzalisha homoni zinazotengeneza maziwa mwilini mwake.

“Hii iambatane na mama kuanza kula vyakula vitakavyosaidia kuzalisha maziwa kwa wingi kama uji, supu na mtori ni kipindi cha kuzingatia lishe bora ili azalishe maziwa kwa wingi yenye ubora zaidi, ili mtoto asifike hatua akasusa,” alisema.

Daktari bingwa wa watoto wadogo, Isabela Herman alisema unyonyeshwaji wa maziwa mchanganyiko, ambapo watoto hulishwa maziwa ya mama na mchanganyiko au maziwa ya wanyama ndani ya miezi sita ya kwanza, huwa na athari mbaya ya kupunguza utoaji wa maziwa ya mama kwa sababu uzalishwaji wa maziwa ya mama hujitngeneza kulingana na kasi ya kunyonya,” alisema.

Dk Isabel alisema ulishaji mchanganyiko chini ya umri wa miezi sita pia unaweza kubadilisha microflora yao ya matumbo na kusababisha kukoma kwa kunyonyesha ikiwemo mtoto mwenyewe kususa ziwa.

Rais mteule wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Mugisha Nkoronko alisisitiza kinamama kunyonyesha kwa kuwa inakuza kupona kwa mtoto haraka wakati wa ugonjwa na inabaki kuwa chanzo muhimu cha virutubisho kwa ukuaji na maendeleo ya afya.

“Muda mrefu wa kunyonyesha una faida nyingi za kiafya kwa wanawake, pamoja na kupunguza hatari za saratani ya matiti na ovari na ugonjwa wa sukari. Kumlisha mtoto kwa chuchu ya chupa huongeza hatari kwa watoto kuugua mara kwa mara,” alisema Dk Nkoronko.

Ofisa lishe mwandamizi kutoka Taasisi ya chakula na lishe TFNC iliyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dorice Katana alisema katika kipindi cha miezi sita ndipo mtoto anatakiwa kuanzishiwa vyakula

Sababu za kususa ziwa

1. Kushindwa kunyonya chuchu ya mama vizuri/chuchu kutokaa vizuri ndani ya mdomo.

2. Amepata mkazo wa misuli katika upande mmoja wa shingo hivyo huumia akinyonya katika ziwa mojawapo.

3. Ana maumivu mdomoni sababu ya vidonda au maambukizi.

4. Amepata maambukizi kwenye masikio au anaota meno, muwasho kwenye koo au mafua.

5. Mtoto ameogopeshwa na jinsi mama alivyochukia baada ya kumng’ata wakati ananyonya.

6. Mama amepunguza utoaji wa maziwa au anatoa maziwa kidogo kidogo.

7. Kubadilika kwa ratiba ya mama. Hii hutokea kama anakwenda kazini, mabadiliko yanayochangia mtoto kugoma kunyonya.

8. Hapendi harufu ya marashi ya mama anayotumia,hupenda harufu asili ya mama hivyo ni vema kutotumia marashi yenye harufu kali.

9. Kuna mabadiliko ya ladha ya ziwa ambayo huweza kusababishwa na mama kurudi kwenye mzunguko wake wa hedhi, vyakula anavyotumia au dawa.

10. Mama ana uvimbe kwenye ziwa hii hufanya ladha ya maziwa kuwa ya chumvi chumvi zaidi hivyo kumkera mtoto.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live