Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi ndivyo vyakula unavyopaswa kuzingatia, unapofikisha umri wa miaka 40

Vyakula Pic Vyakula vya kuzingatia ukifikisha miaka 40

Sat, 11 Jun 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Umeshawahi kufikiria kwa nini watu wengi kuanzia umri wa miaka 40 na kuendelea, huwa wanakumbana na changamoto mbalimbali za kiafya?

Miongoni mwa changamoto hizo ni kukabiliwa na magonjwa yasiyoambukiza kama figo, moyo, kisukari na unene kupita kiasi kutokana na ulaji usiozingatia taratibu ya lishe bora.

Licha ya umuhimu wa lishe bora kwa binadamu, bado yapo mambo mengi ya kuzingatia, kati ya watu wenye umri kuanzia 40 ili kujenga miili yao.

Kwa mujibu wa tovuti ya “Healthy Eating”, watu wenye umri kuanzia 40, wanapaswa kutumia vyakula kama maziwa yanayotokana na mimea, karoti, matunda na protini kama maharagwe ya soya.

Pia, tovuti ya “Holmes place” imeeleza baadhi ya vyakula wanavyopaswa kuvitumia kuwa ni viungo mbalimbali kama tangawizi.

Hata hivyo, licha ya umuhimu wa lishe kwa mwili wa mwanadamu, wataalamu mara nyingi hutoa elimu juu ya faida za lishe bora na kiwango cha chakula ambacho mtu anapaswa kula kwa ajili ya afya yake.

Ofisa Lishe Wilaya ya Temeke, Dk Charles Malale anasema mtu aliyefikisha miaka 40 au zaidi anapaswa kutumia mlo kamili ambao una mchanganyiko wa makundi yote matano ya vyakula.

Makundi ya vyakula ni nafaka kama mizizi na ndizi, kundi la pili ni jamii ya kunde na vya asili ya wanyama mfano maharagwe na kundi la tatu ni jamii ya mbogamboga zinazojumuisha majani ya maboga, kunde, matembele, mchicha, sukuma-wiki, spinachi, kisamvu, mchunga, figiri, mnavu na mlenda.

Kundi la nne ni matunda mfano mapera, mabungo, embe, machungwa pamoja na kundi la tano ni mafuta na sukari.

Pamoja na kuwa mtu huyo atatumia mlo kamili wenye mchanganyiko huo wa makundi yote matano ya chakula, ni lazima awe anatumia zaidi vyakula vinavyojenga na kuimarisha mwili kutoka katika makundi hayo matano.

“Matumizi zaidi ya mboga mboga kwa watu wenye umri tajwa huwasaidia zaidi kwa kuwa huwa na madini na vitamini vinavyosaidia kulinda na kuimarisha mwili,” anasema Dk Malale.

Pia, anasema kadiri umri unavyozidi kwenda mfumo wa umeng’enyaji chakula na utendaji wake wa kazi hupungua, ndio maana watu wenye umri huo hushauriwa kutumia vyakula rahisi kumeng’enywa.

“Wanapaswa kutumia nafaka zisizokobolewa kama mahindi, mtama, ulezi, ngano, mimea jamii ya kunde hasa maharagwe ya soya pamoja na matumizi ya matunda,” anasema Dk Malale.

Pia, anasema watu wanatakiwa kupunguza kula vyakula vinavyo hifadhiwa kwenye makopo. “Kupunguza kiwango cha chumvi katika chakula, hata kupunguza matumizi ya nyama, karanga na siagi,” anasema Dk Malale.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), kupunguza magonjwa yasiyoambukiza ni kupunguza matumizi ya tumbaku na pombe, kuboresha lishe na kufanya mazoezi ya mwili.

Mtaalamu wa Lishe kutoka Hospitali ya Muhimbili, Asina Yusuf anasema mtu mwenye umri kuanzia 40 anahitaji lishe bora itakayomfanya kuwa na afya pamoja na nguvu.

“Wanatakiwa kuepuka vyakula vya kukaangwa kwa kuwa huleta madhara katika mwili endapo wakitumia kwa wingi.

Anasema mbadala wa mapishi ya kukaanga ya kuku, samaki, nyama, ndizi, viazi ni kuoka na kuchoma.

“Watu waachae kufurahia ladha ya mafuta mengi, badala yake watumie viungo vya chakula kuboresha ladha na wapike kwa mafuta kidogo,” anasema.

“Kwa kutumia vyakula hivyo husaidia kupunguza hatari ya kupata magonjwa sugu yasiyoambukiza.

Pia, anasema inashauriwa kupunguza au kuacha pombe aina zote za soda na sharubati bandia kwa kuwa huongeza hatari ya kupata magonjwa sugu yasiyoambukiza.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz