Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi ndivyo sheria inavyomlinda mtoto mfanyakazi za nyumbani

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sheria ya ajira pamoja imeweka umri wa miaka 14 kama kiwango cha chini kiumri kuajiriwa. Hivyo ni rahisi kujibu swali la iwapo mtoto anaweza kuajiriwa kama mfanyakazi za nyumbani. Kwamba anaweza kuajiriwa. Makala haya yatakupeleka katika sheria juu ya ajira za mtoto na kukutanabaishia – ajira hizo ziweje.

Kazi nyepesi. Ingawa sheria inasema mtoto mwenye umri wa kuanzia miaka 14 ana haki ya kufanya kazi, inakwenda mbali kutaka aajiriwe kufanya ‘kazi nyepesi’ na kupata malipo stahiki. Ieleweke kuwa kazi nyepesi ni zile ambazo haziathiri afya ya mtoto, hazikwamishi maendeleo yake kielimu au makuzi yake. Hii ni pamoja na kazi ambazo hazina madhara katika utendaji wa kazi za kimasomo zinazotolewa ili azifanye akiwa nyumbani, haki yake ya kucheza, au kazi ambazo haziathiri uhuru wake wa kushiriki katika mafunzo ya kijamii.

Kwa hali hiyo, mtu haruhusiwi kumwajiri mtoto katika kazi yoyote ile ya kinyonyaji. Pia sheria inasisitiza kuwa, mtu haruhusiwi kumwajiri mtoto katika kazi yoyote ambayo ni hatari katika afya yake, elimu, akili, maumbile na hata katika maendeleo yake ya kiroho! Umesoma vyema, kiroho – apate wasaa wa kuabudu kwa imani ya familia anakotoka.

Muda wa kazi. Sheria inatamka wazi kuwa kazi itakuwa ya kinyonyaji kwa mtoto endapo kazi hiyo itakuwa inazidi masaa sita kwa siku, hailingani au inazidi umri wake, inamlipa mtoto malipo kidogo na yasiyostahili au kazi hiyo inamhitaji mtoto kufanya kazi nyakati za usiku ambazo huanza muda wowote kati ya saa mbili za usiku hadi saa kumi na mbili za asubuhi. Yaani iwapo umemwajiri mtoto mwisho wa kufanya kazi katika siku ni saa mbili za usiku na mwache alale mpaka walau saa moja asubuhi na afanye kazi kwa muda wa saa sita tu kwa siku.

Kazi hatarishi kwa mtoto. Hizi ni zile kazi zinazomfanya au kumlazimisha mtoto aingie baharini, zinazomfanya mtoto au kumlazimisha mtoto aingie mgodini au kwenye machimbo ya mawe, zinazomfanya au kumlazimisha mtoto kuponda mawe, zinazomwingiza au kumlazimisha aingie katika viwanda ambavyo madawa huzalishwa au kutumika, kazi za baa, hoteli, na mahali pengine popote pa starehe na mwisho ni kazi ambazo zinamweka mtoto katika mazingira ya jinsia ya mahusiano ya kingono au ukahaba bila kujali kama analipwa au halipwi.

Kuhusu wasichana na wavulana wasaidizi wa kazi za nyumbani. Uzoefu tulionao unaonyesha kwamba familia nyingi zinazoishi mijini huhitaji wasaidizi wa kazi za ndani, wa kike (house girl) ama wa kiume (house boy / shamba boy). Wengi wa waajiri katika kundi hili pasipo kujua ama kwa kujua huajiri watoto wenye umri chini ya miaka 14. Hili ni kosa na katika sheria, haijalishi ulifahamu ya kuwa ni kosa au la.

Kundi la pili la waajiri hawa huwa makini kutaka kuajiri walau mwenye umri wa kuanzia miaka 14 na kuendelea. Hawa pia wanaweza kujikuta wanaingia katika kosa la unyonyaji na lile la muda wa kazi kwa mtoto mwajiriwa.

Kundi la tatu ni wale tunaompatia mtoto ajira bila ya kujua historia yake. Yaani amefikaje mjini, aliletwa na nani na je nyumbani kwao wajua aliko na anafanya nini huko? Hili laweza kuwa kosa la usafirishwaji haramu wa watoto. Watoto wengi wakimaliza elimu ya msingi vijijini hurubuniwa na madalali kutafutiwa shule kujiendeleza au kazi mijini. Watoto hawa huishia majumbani mwetu pasi sisi kujua wamefikaje mijini.



Chanzo: mwananchi.co.tz