Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hiki ndio chanzo kikuu cha vifo vya uzazi nchini

04d1102f5fdb2eadad41eaa68f065aa8 Hii ndio chanzo kikuu cha vifo vya uzazi nchini

Fri, 24 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TAKWIMU za vifo vya uzazi za Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zilizokusanywa kutoka Januari hadi Desemba mwaka jana, zinaonyesha asilimia 26.3 ya vifo vingi vilisababishwa na kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua.

Kutokana na sababu hiyo, Mpango wa Taifa wa Damu Salama nchini umezindua kampeni ya kitaifa ya kuihamasisha jamii kuchangia damu ili kuokoa vifo kwa wajawazito vinavyotokana na uzazi.

Akizungumzia kampeni hiyo, Mkuu wa Idara ya Ukusanyaji Damu katika Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Dk Avelina Mgasa, alisema kaulimbiu ya kampeni za mwaka huu ni “Changia Damu Kuokoa Wanaoleta Uhai Duniani”.

“Kampeni hii inalenga kuihamasisha jamii kujitolea kutoa damu kwa hiyari ili kuokoa maisha ya akinamama wajawazito wanaotumika kama chombo cha kuleta uhai duniani,” alisema.

Alieleza kuwa kauli mbiu hiyo inatoa hamasa na kuihamasisha jamii kujitolea kuchangia damu kwa hiari ili kuongeza upatikanaji wa damu ya kutosha na salama itakayosaidia kuokoa maisha ya akinamama ambao hupoteza maisha kila siku kutokana na matatizo ya uzazi na wakati wa kujifungua.

Kampeni hiyo iliyozinduliwa katika kanda zote saba za kukusanya damu nchini imeanza juzi na imelenga kukusanya chupa za damu 19,514 kutoka kwenye timu 226 zilizopo nchi nzima ambazo ni asilimia tatu ya malengo yao ya damu kwa mwaka.

Pamoja na hayo, Mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Mashariki inayohusisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro imepanga kufunga kampeni yake ya ukusanyaji damu salama kesho katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ilala, Amana.

Katika ufungaji wa kampeni hizo utakaohusisha taasisi maarufu ya kuhudumia wagonjwa na kuchangia damu ya Jamiiyatul Akhlaaqul Islaam (JAI), itahusisha pia huduma za kuwasaidia wagonjwa na kusafisha maeneo ya hospitali hiyo sambamba na huduma za utoaji damu kwa hiari.

Akizungumzia ufungaji wa kampeni hiyo iliyozinduliwa Septemba 20 mkoani Morogoro, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Mpango wa Damu Salama, Dk Pendalieli Joseph, alisema timu ya watoa huduma kutoka vikundi 15 vitashiriki ili kutoa huduma kwa watoa damu.

Kanda nyingine za Mpango wa Taifa wa Damu Salama ni Kanda ya Ziwa inayohudumia mikoa ya Mwanza, Simiyu, Geita, Mara, Kagera na Shinyanga na Kanda ya Magharibi kwa mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi, na Singida.

Nyingine ni Kanda ya Kusini inayohudumia mikoa ya Lindi na Mtwara; Kanda ya Kaskazini inayohudumia mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Manyara pamoja na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayohudumia mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe, Ruvuma na Iringa.

Katika hatua nyingine, Mpango wa Taifa wa Damu Salama umebadilisha mwelekeo wake wa kuigeukia jamii kwa ajili ya kukusanya damu ili kukabiliana na changamoto ya kutegemea wanafunzi wa shule za sekondari iliyokuwa ikiwatumia.

Dk Mgasa alisema hivi sasa wanaweka mkazo kwa jamii kujitolea damu kwa hiari kwani Mpango wa Taifa wa Damu Salama haujaweza kufikia lengo la kukusanya chupa za damu zinazokidhi mahitaji ya nchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz