Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hiki ndicho kinachovutia mbu kumuuma binadamu

Utafiti: Ugunduzi Wa Bahati Utakavyosaidia Kupambana Na Malaria Hiki ndicho kinachovutia mbu kumuuma binadamu

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ukitaja mbu, wazo litakalomjia mtu kwa haraka ni ugonjwa wa malaria. Hiyo inatokana na mazoea yenye ukweli kwamba, mdudu huyo hueneza ugonjwa huo kama ilivyo kwa malale na matende.

Lakini kuna baadhi ya mambo kuhusu tabia ya mbu ambayo watu wengi hawayafahamu, mbali na sifa yake ya kueneza magongwa, hasa malaria.

Hebu jiulize; hivi umewahi kukaa na wenzako watano lakini ukajikuta ni wewe peke yako ndiye unayelalamika kwamba unang’atwa na mbu?

Kama umekutwa na hali hiyo, basi unaweza kuwa mmoja wa watu walio kivutio kwa mbu.

Kwa kawaida, mvuto hutokana na harufu ya asili inayotoka mwilini mwa mtu anayeshambuliwa zaidi na mbu.

Wanasayansi wanasema kwamba mtu mmoja kati ya watano huwa kivutio cha mbu na kwamba mdudu huyo akinusa harufu ya mtu huyo, hata akiwa na wenzake zaidi wanne, basi atakwenda kwake na kwamba hata akifukuzwa, mbu huyo atarudi na kumuuma tena mtu huyo.

Daktari bingwa wa upasuaji wa Marekani, Joseph Mercola anasema kuwa kuna aina nyingi za mbu, lakini asilimia kubwa ya mbu wenye tabia hiyo ni mbu jike aina ya Anofelesi, ambao pia huambukiza malaria.

Anasema kuwa mbali na tabia hiyo mbu hao huvutiwa na maeneo yenye kemikali kwa kunusa harufu hiyo umbali wa mita 50 kutoka walipo kabla ya kwenda kwenye eneo hilo. Mbu jike ndiyo huvutiwa zaidi na kupenda kunyonya damu ya binadamu kuliko mbu dume.

Dk Mercola ambaye ameandika majarida mbalimbali ya afya, anasema kuwa mbu jike hupendelea kufanya hivyo kwa sababu madini ya chuma na protini wanayonyonya kwenye damu ya binadamu huwasaidia kutengeneza mayai na baadaye kuzaliana.

Kutokana na hilo, wanasayansi wamebaini kuwa mbu huvutiwa na bakteria.

Wanasema binadamu ana bakteria trilioni moja kwenye ngozi, lakini kati ya hao, asilimia 10 tu ndiyo hufanana kwa binadamu wote na asilimia nyingine hutofautiana, hali ambayo huchangia baadhi ya watu kuumwa zaidi na mbu kuliko wengine.

Mazingira

Kwa mujibu wa wanasayansi hao, asilimia kubwa ya mbu huvutiwa zaidi na harufu ya kemikali ya lactic, ammonia, carboxylic na octenol ambazo hutoka kinywani kwa binadamu, kwenye jasho, pamoja na gesi carbon dioxide anayotoa binadamu.

“Kadri unavyotoa hewa yenye gesi ya Carbon dioxide ndipo unavyowavutia zaidi mbu. Kutokana na hilo, watu wanene hung’atwa zaidi na mbu kwa sababu hutoa harufu hiyo zaidi ikilinganishwa na watu wembamba,” anasema Dk Mercola.

Moyo

Kuhusu mapigo ya moyo, mtaalamu huyo anasema: “Kadri moyo wako unavyodunda, ndivyo unavyoweza kuwa kivutio kwa mbu. Mfano, kama unafanya mazoezi na mwili wako ukapata joto sana lazima mbu watakung’ata zaidi hasa ukiwa na pumzi ndogo.”

Dk Mercola anasema mbu huvutiawa na harufu inayotokana na mabadiliko ya kemikali ndani ya mwili wa binadamu.

Anaeleza kuwa mara nyingi mabadiliko hayo hutokea na kusababisha mtu kutoa jasho na harufu ya kipekee.

“Kama unanukia harufu nzuri ambayo ni halisi, mbu hawavutiwi na wewe. Lakini ikitokea unanuka uvundo, basi lazima utakuwa kivutio chao na watakusumbua na kukuuma zaidi,” anasema.

Maelezo ya wanasayansi hao yanaendana na utafiti uliofanywa na wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya Ifakara (IHI), ulioangazia tabia ya mbu hasa harufu, ilipotafiti njia mbadala ya kukinga binadamu dhidi ya wadudu hao.

Watafiti hao walibaini kuwa, mbali na maeneo yenye unyevunyevu, mbu huvutiwa zaidi na harufu ya uvundo. Sehemu au kitu chochote chenye harufu hiyo, huwa na mbu zaidi.

Utafiti huo wa Ifakara, umewawezesha kubuni mbinu mbalimbali za kuuwa mbu, ikiwamo ya ‘mosquito landing box’, ambalo hujazwa vitu vilivyovunda pamoja na kifaa chenye shoti na huwekwa nje ya nyumba ili kuwavutia mbu ambao hufa kwa kupigwa shoti. Boski hilo hufanya mbu wasiingie ndani ya nyumba.

Daktari kutoka Hospitali ya Mwanyamala, Dar es Salaam, Dk Syriacus Buguzi anasema kuwa kuna tafiti kadhaa ambazo zimeonyesha uhusiano uliopo kati ya harufu na tabia ya mbu.

Akitoa mfano wa watu wanaowavutia zaidi mbu anasema: “Moja tafiti zilizowahi kufanywa ni zile zinazohusu wanawake wajawazito, ambao hung’atwa zaidi na mbu kutokana na harufu wanayotoa wakiwa katika hali hiyo.

“Ili kigundua kwa nini kina mama hawa walikuwa wakishambuliwa na malaria zaidi wakati wa ujauzito, iligundulika kwamba hutoa harufu fulani inayowavutia mbu … iliaminika kwamba kina mama hao hutoa jasho lenye kemikali ambayo ina harufu inayovutia mbu.”

Pia, utafiti uliofanywa mwaka 1999 ulibaini kuwa jasho la binadamu likikaa kwa siku mbili huanza kutoa harufu ya uvundo na kuvutia mbu, hasa waenezao ugonjwa wa malaria.

Pia, bakteria wanaotengenezwa kutokana na joto, huoza na kutengeneza kemikali yenye harufu inayowavuatia mbu.

Kadhalika, mbu huvutiwa na harufu ya joto linalotoka kwenye miguu, baada ya kuvaa viatu kwa muda mrefu. Daktari huyo anasema hata ikitokea mtu amevua soksi na kuzihifadhi bila kuzifua, mbu watajaa katika sehemu hiyo kutokana na harufu.

Hata hivyo, Dk Buguzi anasema mbali na mbu kuvutiwa na harufu hizo, kuna wakati pia mwili wa binadamu hutoa harufu ambayo huwafanya wakimbie.

Anasema harufu hiyo ambayo kitaalamu huitwa ‘methylpiperzine’ ndiyo wataalamu waliyotumia kutengeneza dawa ya kufukuza mbu inayoitwa kitaalamu ‘DEET’ (N,N-diethyl-meta-toluamide)

Watu wanaotoa kamikali ya ‘1-methylpiperzine’ hawafuatwi na mbua kama ilivyo kwa wale ambao hawatoi kemikali hiyo.

Unawezaje kujikinga

Dk Mercola anabainisha kwamba namna bora na ya asili ya kujikinga na mbu ni kukaa ndani ya nyumba, ambako hakuna mbu.

Anasema ukikaa nje hasa sehemu zenye unyevunyevu ambazo mbu hupendelea lazima watakung’ata.

“Hakikisha unafanya usafi wa mazingira nje ya nyumba yako na kusiwe na unyevunyevu,” anasema.

Taasisi ya Kuzuia Mbu ya Marekani (AMCA) ilianisha njia nyingine zinazoweza kusaidia watu kujizuia kuumwa na mbu ambazo ni pamoja na kusafisha mazingira na kuondoa madimbwi ya maji nje ya nyumba.

Pia, kuvaa mavazi ambayo hayaachi baadhi ya sehemu za mwili wazi kama miguu na mikono kwa kuwa maeneo hayo yakifunikwa vizuri siyo rahisi mbu kuuma.

Dk Janet Hull wa Marekani anasema utafiti uliofanyika mwaka 1960 ulibainisha kuwa, unywaji wa vidonge vya Vitamini B1 unasaidia kufukuza mbu asimuume binadamu.

“Matone hayo husaidia mwili kutoa hafuru ambayo huwafanya mbu wasimsogelee binadamu huyo,” anasema.

Dk Hull anasema kunywa kidonge kimoja cha Vitamini B1 kwa miezi saba ni njia nzuri inayoshauriwa na wataalamu wa afya ili usiumwe na mbu.

Anaongeza kuwa ulaji wa vitunguu swaumu mara kwa mara pia husaidia kutoa harufu ambayo hufanya mbu wakimbie wanapokaribiana na mtu mwenye harufu hiyo.

Ufanyaje?

Daktari wa tiba ya magonjwa ya binadamu, Samweli Shitta anasema mbali na mbu waenezao malaria, kuna aina nyingi za mbu.

Anasema baadhi ya watu wakiumwa na mbu huvimba, wengine huwashwa na wengine hupata vipele au harara ambazo huacha makovu kwenye ngozi.

“Kuna mbu waenezao ugonjwa wa matende, kuna wengine wakikung’ata unawashwa, unapata upele na wengine kupata uvimbe kwa sababu ngozi zinatofautiana,” anasema.

Anasema ikiwa mtu amepatwa na hali hiyo anaweza kutumia dawa za kutibu mzio, ambazo husaidia kupunguza muwasho, kuondoa harara pamoja na alama zinazoweza kutokea kwenye ngozi.

Dk Mercola anaongeza kuwa, njia nyingine ni kutumia dawa za asili kama mdalasini kwa kuchanganya na asali, kisha kupaka mwilini, mafuta ya mzeituni, sabuni ya ‘citronella’ na mafuta ya nazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live