Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii ndiyo hatari kwa wanaume wanaokalia pochi zilizojaa

94027 Pic+pochi Hii ndiyo hatari kwa wanaume wanaokalia pochi zilizojaa

Mon, 3 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hakuna ubishi baadhi ya wanaume hutumia wallet (pochi) kuhifadhia fedha, kadi za matibabu na za benki, bila kujua madhara wanayoweza kuyapata endapo watazikalia.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojino maalumu, Daktari wa Ubongo na Uti wa Mgongo kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), Nicephorus Rutabasibwa anasema mtu akikalia pochi ambayo haina kitu au haijajaa hawezi kupata madhara, lakini ikiwa imejaa vitu huwa na madhara. “Unaposema umekalia pochi ambayo haijajaa kwa maana kuwa haijatuna, inakuwa haina uhusiano wowote na maumivu ya mgongo,” anasema Dk Rutabasibwa.

“Badala yake ile pochi itakuwa inakandamiza tu ule mfupa mkubwa wa kiuno na sehemu hiyo huwa kuna mfupa wa paja ambao unakuwa haujaenda kwenye mgongo; hivyo hakuna madhara hapo.”

Lakini, anasema kuna mshipa wa fahamu ujulikanao kitaalamu kama Sciatic Nerve, unaotoka kwenye uti wa mgongo kuelekea mguuni, kupitia kwenye mfupa wa kiuno.

“Sasa kama umeweka wallet iliyotuna sana katika mfuko wa nyuma wa suruali uliyovaa na ukakaa nayo, basi ule uzito unaweza kukandamiza mshipa wa Sciatic Nerve na kusabisha ganzi na maumivu kwenye mguu; pia, unaleta maumivu katika mgongo kwa sababu mshipa huo unakuwa umeshatoka kuelekea kwenye mguu.”

Dk Rutabasibwa anasema madhara mengine anayoweza kupata mtu kama atakalia pochi iliyojaa ni kupata ganzi katika miguu, pindi anaposimama au kupata maumivu yanayoambatana na ganzi.

Pia Soma

Advertisement
“Hivyo, siwezi kusema kuweka wallet nyuma ya mfuko wa suruali ni vibaya iwapo haijajaa vitu yaani haijatuna, isipokuwa mtu anaweza kupata madhara kama itakuwa imetuna kupitiliza,” anabainisha.

Wakati Dk Rutabasibwa akieleza hayo, Dk Salvatory Florence kutoka Hospitali ya Hubert Kairuki Memorial( HKMH), anasisitiza kuwa mwanaume anayekalia pochi iliyojaa kwa muda mrefu anakuwa katika hatari ya kupata maumivu ya mgongo na kiuno yasiyoisha.

Dk Florence anasema mkao mbaya usiozingatia afya ya mgongo, ni miongoni mwa mambo yanayochangia mtu kupata maumivu ya kuino na mgongo yasiyoisha.

“Mwanaume akikalia pochi yake ambayo ameiweka katika mfuko wa nyuma wa suruali, anakuwa hawezi kukaa vizuri na matokeo yake anakuwa amekaa upande, hivyo kadri atakavyokuwa anakaa hivyo kwa siku nyingi husababisha pingili za mgongo zinazotakiwa kunyooka, kupinda,” anasema Dk Florence.

“Maumivu ya mgongo, wakati mwingine hutokea katika miguu, kiuno kutokana na pingili kupinda; zile pingili zinakandamiza neva za fahamu, pia unaweza kupata maumivu ya uti wa mgongo baina ya pingili kwa kuwa kuna sehemu ambayo ni laini.”

Pia, anasema hali hiyo inavyoendelea na muda unavyokwenda wanaume hupata maumivu ya mgongo ya kudumu.

Madhara mengine ni upungufu wa nguvu za kiume

Pia anasema maumivu ya kiuno baadaye huwa ni ya kudumu; na hali hiyo ikiongezeka inaweza kusababisha mwanaume kushindwa kubana vizuri mkojo.

“Madhara mengine ni kusababisha upungufu wa nguvu za kiume kutokana na kukandamizwa kwa neva za fahamu,” anasema Dk Florence.

Anasema madhara mengine ni miguu kuhisi kama inawaka moto na hata ukitumia dawa za kupunguza maumivu mara nyingi huwa hayaishi.

Watu wengine walio katika hatari ya maumivu ya mgongo

Mbali na kukalia pochi, Dk Rutabasibwa anasema kuna mambo matatu yanayosababisha madhara katika uti wa mgongo kwa binadamu.

Anasema kundi la kwanza ni la watu wanaobeba mizigo mizito (makuli).

“Hapa tunaangalia mtu anayebeba mizigo mizito ( kuli) wenye uzito wa tani nne hadi nane kwa muda wa saa nane kwa siku, katika kipindi cha miaka minane na kuendelea, mtu huyu anaweza kupata matatizo ya uti wa mgongo wa binadamu,” anasema Dk Rutabasibwa.

Kundi lingine la watu ni wale wanaofanya kazi kwa mkao wa kujikunja (Awkward Posture).

“Awkward Posture inawahusu wale watu wanaochomelea chuma ndani ya meli au ndani ya mabomba mkubwa, mara nyingi mafundi hawa wanakuwa wamechuchumaa au wameina huku wanachomelea,” anaeleza.

Kundi la tatu ni la watu wanaohamisha bidhaa au mzigo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine huku wakiwa wameina.

“ Mfano mzuri katika hili, ni wale wanaopanga mifuko ya saruji atanyanyua mfuko huo atapanga, ataenda kuchukua tena mwingine na kupanga, hapo akifanya kazi hiyo kwa muda mrefu itamleta madhara katika uti wa mgongo” anaeleza.

Wanachosema wanaume

“Mwaka juzi nilikuwa nasumbuliwa sana na mgongo unauma na kuacha; miguu kuwaka moto, nikaenda duka la dawa wakanipa dawa nikaendelea vizuri,” anasema Isack Brown ambaye ni fundi nguo anayetumia cherehani.

“...lakini baada ya muda wa miezi sita kupita hali ile ya maumivu ya mgongo ilianza tena, nikaamua kwenda hospitali tu,” anasema Isack Brown ambaye ni fundi cherehani.

Brown anasema hospitali aliambiwa ana tatizo la mgongo, lililosababishwa na mkao mbaya usiozingatia afya ya mgongo.

Brown anasema: “Walinieleza hali hiyo inatokana na mimi kupenda kuweka wallet iliyotuna katika mfuko wa nyuma wa suruali yangu na kuikalia; hivyo uzito wa ile wallet ulikandamiza mishipa iitwayo Sciatic Nerve na kunisababishia ganzi na maumivu kwenye mguu na kwenye mgongo.”

Peter Moses mkazi wa Kimara, anasema yeye ni mdau wa wallet lakini huwa anaiweka kwenye mfuko wa shati au suruali kwa mbele. “Mwanzo nilikuwa naweka mfuko wa nyuma, lakini nikawa naona kama inakera upande mmoja,” anasema.

Nini kifanyike

Dk Philemon Kalugira kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga anasema maumivu ya mgongo ni ile hali ya kuhisi maumivu au kutojisikia vizuri katika misuli au mifupa ya mgongo wako (eneo lililopo kati ya kiuno na shingo).

Anasema maumivu haya yanatofautiana baina ya mtu na mtu; pia yanategemea wapi ilipo shida katika mgongo wako; kwa maana ya kwamba nini kisabisha na kiungo gani kilichoathiriwa.

Dk Kalugira anasema hata dalili nazo hutegemea na kisababishi, hivyo baadhi ya watu huwa na dalili zinazofanana huku wengine wakiwa na dalili za aina mbalimbali na kushindwa kufanya shughuli za kawaida za kila siku kutokana na maumivu.

Anashauri wanaume kuweka pochi zao sehemu nyingine na si katika mfuko wa nyuma wa suruali.

“Pochi zao wanaweza kuweka katika mfuko wa koti au suruali kwa mbele,” anasema.

Chanzo: mwananchi.co.tz