Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii ndio halisi ya Bima ya Afya Tanzania

Bimapicttt.png Hali halisi ya bima afya Tanzania

Sat, 30 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Licha ya umuhimu wa kujiunga na bima ya afya ili kuepuka gharama za matibabu za papo kwa hapo katika hospitali, kituo cha afya na zahanati, hadi sasa ni Watanzania wachache waliojiunga kwenye mfumo huo.

Bima ya afya kwa wote bila vikwazo vya kiuchumi (UHC) ni huduma inayopendekezwa kwa sasa ili watu wote nchini watibiwe bila kutatizika kifedha.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Afya, Edward Mbanga anasema Watanzania waliopo kwenye mfumo wa bima ya afya ni 8,264,271 licha ya nchi kuwa na watu milioni 55.

Anasema kwa mujibu wa takwimu za makadirio ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), hadi mwaka jana ni asilimia 14.7 pekee ya Watanzania waliojiunga.

Kutokana na takwimu hiyo, asilimia 85.3 ya Watanzania hawajajiunga na huduma ya bima ya afya.

Mbanga anatoa mchanganuo wa idadi hiyo ya wanufaika akisema wamegawanyika katika makundi tofauti, huku idadi kubwa ya wanufaika ikionekana ipo katika mifuko ya umma kwa maana ya Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

“Bima ya NHIF imewakusanya watumishi wa umma na wachache walioingia (ambao sio watumishi wa umma), jumla yao inakuwa asilimia 8, mfuko wa CHF iliyoboreshwa wanufaika wapo asilimia 5.4, bima za afya binafsi ni asilimia moja na wale waliojiunga kupitia NSSF ni asilimia 0.3,” anasema Mbanga.

Alivyoulizwa kupungua kwa takwimu za mwaka 2019 zinazoonyesha asilimia 33 walikuwa na bima ya afya, Mbanga anasema, “katika bima wengi wanalipia kila mwaka, sasa unakuta mwingine anakuwa halipi, kwa hiyo anaondoka katika mfumo, ndiyo maana kuna kupanda na kushuka kwa takwimu.”

Hata hivyo, Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote unatarajiwa kuwasilishwa na kusomwa bungeni katika mkutano wa Bunge unaoanza Novemba 2 mwaka huu jijini Dodoma.

Akizungumzia hilo, Mbaga anasema muswada huo unaharakishwa hivi sasa kupelekwa bungeni baada ya taratibu muhimu kukamilika.

Matarajio ya Serikali

Mkurugenzi wa Afya Tamisemi, Dk Ntuli Kapologwe anasema hivi sasa huduma ya bima ya CHF inahusisha watu wasio katika mfumo rasmi wa ajira kwa maana ya wakulima, wajasiriamali na wafanyakazi, huku walionufaika hivi sasa ni milioni 3.3.

“Katika makusanyo tumefikia Sh19 bilioni. Mfuko huu unawalenga wakulima, wajasiriamali, wafugaji na wafanyakazi, mwamko ni mkubwa sana, kuanzia Januari mpaka sasa wengi wamejitokeza na kujiunga, inagharimu Sh30,000 kwa familia ya watu sita kwa mwaka,” anasema Dk Kapologwe.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima anasema muswada wa sheria hiyo unatarajiwa kusomwa Bungeni Novemba mwaka huu na utahusisha Bunge kujadili sheria ya Bima ya Afya kwa wote.

“Tunatoka kwenye uhiari tunakwenda kwenye ulazima. Katika hili pia tutaangalia namna gani kundi la wasiojiweza linaingizwa kwa kuwa watu wana viwango tofauti vya uchumi. Zimetengwa Sh149.7 bilioni, lengo lake ukionekana familia yako haina uwezo wewe utalipiwa.

“Tunajua huwezi kuwalipia wote, tutachukua asilimia 30 tutawalipia tutawawekea utaratibu wa msamaha, Tasaf (Mfuko wa Maendeleo ya Jamii) watatusaidia kuchukua kaya nyingine kumuunga mkono Rais,” anasema Waziri Gwajima.

Hata hivyo, NHIF imesema ipo tayari kutekeleza jukumu la kuratibu mchakato wa bima ya afya kwa wote iwapo muswada unaotarajiwa kwenda bungeni ukipitishwa kuwa sheria.

Kwa sasa mfuko huo upo katika hatua za mwisho za kufanya mapitio ya kitita cha matibabu ili kuongeza wigo kwa wanachama wa mfuko huo katika kupata huduma zaidi na bora.

Vipi kuhusu mifuko ya bima

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga anasema mchakato huo ni wa muda mrefu na wenye manufaa kwa wanachama na Watanzania kwa jumla.

Anasema Serikali imekuwa ikizungumzia ujio wa bima ya afya kwa wote na imewekeza kwanza kwa kuimarisha miundombinu, ikiwamo ujenzi wa hospitali za kutosha, imeongeza bajeti ya dawa, miundombinu ya kutosha.

“Serikali imeshaweka wazi Bunge litatunga sheria itakayosimamia suala hilo na tumeshamsikia Rais Samia Suluhu Hassan amesema hicho ni kipaumbele chake, nasi tumeshajiandaa sheria itakapokuja lazima mfumo uwe vizuri.

“Kama mfuko wa umma tumeshajipanga namna gani tutaweza kushirikiana na kutoa huduma kwa wananchi wote na tunaamini tutaweza, miaka 20 tuliyokuwepo katika soko la bima ya afya inatutosha kulibeba hili jukumu,” anasema Konga.

Pia, anasema wakati mfuko ukitimiza miaka 20 wameanza kuboresha huduma na kuongeza ushirikishwaji kwa nia ya kuwapa huduma nzuri na bora wanachama wake na watoa huduma wao.

Konga anasema kwa sasa, kitita cha matibabu cha NHIF kinajumuisha ada ya kujiandikisha na kumwona daktari, huduma za kulazwa, huduma za dawa, vipimo vya maabara na uchunguzi (X-Ray, Echo na EEG, Ultrasound), huduma za kinywa na meno (kung’oa na kuziba meno), huduma za uzazi (kujifungua kawaida na kujifungua kwa upasuaji).

Pia, anasema wanatoa huduma za matibabu ya kibingwa na huduma za upasuaji mdogo na mkubwa.

“Mfuko umepiga hatua kubwa tangu ulipoanzishwa Julai Mosi, 2001, wakati ulipoanza na vituo ya kutoa huduma 300 vyote vikiwa vya umma, lakini sasa una vituo zaidi ya 8,500, vikiwamo vya umma, sekta binafsi na vya taasisi za dini vinavyowahudumia wanufaika wa mfuko ambao wamefikia milioni 4.8,” anasema.

Mwenyekiti wa Umoja wa Watoa Huduma Binafsi za Afya Tanzania, Dk Egina Makabwe anasema umoja huo na watoa huduma wake hawapingi suala la Serikali kuja na bima ya afya kwa wote na wataendelea kushirikiana nayo kutoa huduma bora za afya nchini.

“Vituo vya afya binafsi vinaunga mkono juhudi za Serikali za bima ya afya kwa wote, sisi hatuwezi kuupinga huu mpango, ni mpango mzuri na tunahitaji kila Mtanzania aweze kupata huduma za afya, sisi tunafanya kazi kwa pamoja na Serikali ili kuwawezesha wananchi wote wapate huduma,” anasema Dk Makabwe.

Pia, anasema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakihudumia wanachama wa bima za afya, wakiwamo NHIF, hivyo mabadiliko yaliyokuwepo katika mfuko huo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha hatua hiyo.

“Ukiangalia miaka ya nyuma kidogo mfuko huu ulitoa huduma kwa kundi dogo, lakini kutokana na mabadiliko yaliyofanyika, ikiwamo usajili wa vituo vingi zaidi, kuongeza ufanisi wa uchakataji wa madai kwa watoa huduma sasa tunalipwa ndani ya siku 40,” anasema Dk Makabwe.

Pia, anasema changamoto ya ugonjwa wa Uviko-19 imesababisha kuwapo kwa upungufu wa rasilimali watu katika sekta ya afya, pia gharama kubwa za uendeshaji, ingawa kwa sasa hali imekuwa na nafuu.

Mmoja wa wanachama wa mfuko huo, Japhet John anasema hali ya utoaji huduma ilivyokuwa awali imeboreshwa kwa kiasi kikubwa.

John anasema huduma nyingi zimeongezwa, ikiwamo kulipia matibabu ya magonjwa sugu. “Uwepo wa vifurushi umesaidia sisi wengine kujiunga na familia zetu, natumia Wekeza Afya, nimeweza kuingia huko na sasa situmii fedha ya mfukoni kwenye matibabu ikitokea mke, mtoto au mimi naumwa kila kitu bima inalipa,” anasema.

Chanzo: mwananchidigital