Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Haya ndiyo yanayochangia wazazi kupuuza chanjo ya surua kwa watoto

63846 Chanjo+pic

Sat, 22 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati Serikali ikiendelea kuhamasisha watoto wapatiwe chanjo ya surua rubella kwa manufaa ya afya zao, imebainika kuwa baadhi ya wazazi huwapeleka watoto katika chanjo ya surua ya kwanza tu, kisha hawawapeleki tena.

Chanjo hiyo kwa mara ya kwanza hutolewa wakati mtoto akiwa na miezi tisa na ya pili anapofikisha mwaka mmoja na nusu.

Surua ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo vingi vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano hasa kwa nchi zinazoendelea, ndiyo maana wataalamu wa afya wanashauri watoto wapatiwe chanjo ili kukabiliana na hatari hiyo.

Mratibu wa chanjo jijini Tanga, Hamza Maulid anasema chanjo inapotolewa mara ya kwanza muitikio huwa ni mkubwa lakini kwa mara ya pili hupungua.

Anasema changomoto iliyopo ni wazazi kutofika kwa wakati katika chanjo hasa zile tarehe walizopangiwa kurudi kliniki, hivyo kusababisha kuvurugika dozi iliyotolewa awali kwa mtoto.

Takwimu za chanjo ya surua rubella Tanga

Pia Soma

Kwa mujibu wa taarifa kutoka idara ya afya ya takwimu; kuanzia mwaka 2016 hadi 2018, Jiji la Tanga limeweza kufikia asilimia 100 ya uchanjaji huku lengo la kimataifa ni asilimia 95.

Mwaka 2016 watoto waliopata chanjo ya surua rubella ya kwanza ni 9,148 na wasiopata walikuwa 1,874.

Kwa mwaka huo, awamu ya pili waliopata chanjo ni 7,689 na waliokosa 3,333.

Mwaka 2017 watoto waliopata chanjo hiyo awamu ya kwanza walikuwa ni 10,155 wasiopata walikuwa 1,240 huku awamu ya pili waliopata ni 9,557 na wasiopata ni watoto 1,838.

Kwa mwaka 2018 jumla ya watoto waliopata chanjo awamu ya kwanza ni 12,082 na hakuna ambaye hakupata.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, awamu ya pili kwa mwaka huo watoto waliopata walikuwa 11,035.

Taarifa hizo zinaonyesha kuwa, mwaka jana Tanga ilipita malengo waliyowekewa na Serikali utoaji chanjo licha ya wazazi kukwepa chanjo ya pili.

Hadi sasa kuna vituo 52 vinavyotoa huduma ya chanjo ya surua katika Jiji la Tanga. Hata hivyo, Maulid ambaye ni mratibu wa chanjo, anasema halmashauri imejipanga kupita nyumba kwa nyumba katika vijiji vilivyo mbali na vituo vya kutolea huduma hiyo ili kuwafikia watoto wote waliopo Tanga.

Kwa nini wazazi hukwepa chanjo kwa watoto?

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu kutowapeleka watoto kupatiwa chanjo, wazazi wanasema wanakatishwa tamaa na lugha mbaya kutoka kwa wauguzi katika vituo vya afya. “Ni kweli wakati mwingine hatuhudhurii kliniki kwa wakati kwenye chanjo hizo, lakini siyo kwa kupenda bali ni kutokana na lugha chafu tunazopewa na wauguzi. Tunaona aibu maana wengine hubeba mimba watoto wao wakiwa wadogo,” anasema Mariam Shabani, mkazi wa Mwanzange.

Asha Hussen, mkazi wa Kange Kasera, anasema anatambua kuwa chanjo ni muhimu kwa afya ya mtoto lakini kitu kinachosababisha asirudi kliniki ni kutokana na shughuli nyingi za nyumbani na shambani zinazomkabili, hivyo kushindwa kwenda kumpeleka mtoto kupata chanjo hata kama tarehe yake imefika.

Mkazi wa Chumbageni, Mwanakombo Jumaa anasema wazazi wote ambao hawawapeleki watoto kupata chanjo wanafanya uzembe kwa sababu licha ya kufahamu kuwa ni umuhimu katika kulinda afya za watoto wao, lakini wanapuuza.

Mmbonea Mnyone anasema sababu kubwa ya wazazi (wanaume na wanawake) kutowapeleka watoto kupatiwa chanjo ni ukosefu wa elimu kuhusu umuhimu wa chanjo hizo.

Mnyone anasema baadhi ya wazazi hawajaelimishwa sawa sawa kuhusu afya ya uzazi na umuhimu wa chanjo kwa watoto.

George Abraham anaishauri Serikali kuona umuhimu wa kutoa elimu kwa wajawazito ili watakapojifungua waanze kliniki bila kukosa.

Wataalamu wa afya wanasemaje?

Daktari bingwa wa kinga na tiba ya macho katika Zahanati ya City, Athuman Ngereza anasema chanjo ya surua inatolewa ili kuzuia watoto wasipate magonjwa nyemelezi ya nimonia, ngozi, macho na masikio.

Dk Ngereza anasema surua inasababisha vifo hasa kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.

“Unaweza kuona mtoto macho yake kama yana watoto ndani, hiyo inatokea kwa sababu ya kuugua surua kwa muda mrefu, surua husababisha madhara mengi homa ya mapafu na uti wa mgongo,” anasema Dk Ngereza.

Pia, anasema Tanzania kuna utaratibu wa kuwapeleka watoto kliniki tangu anazaliwa mpaka anafikisha miaka mitano; hivyo aliwataka wazazi watumie fursa hiyo kuwapeleka watoto kupata chanjo ya surua ili kuepuka magonjwa yanaweza kujitokeza kwa mtoto.

Muuguzi wa Kituo cha Afya cha Ngamiani, Asna Mrunguza anasema hakuna lugha yoyote mbaya wanayowapatia wazazi pindi wanapohudhuria chanjo bali wanawaeleza umuhimu wake na kurudi kwa wakati kliniki pindi wanapoandikiwa tarehe.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) dozi mbili za njano za surua ni muhimu katika kuwalinda watoto na magonjwa.

Shirika hilo limeeleza kuwa takribani watoto 110,000 duniani, walifariki dunia mwaka 2017 kutokana na ugonjwa wa surua, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 kutoka mwaka 2016.

UNICEF inaeleza kuwa katika miezi mitatu ya kwanza mwaka huu, matukio 168,000 ya ugonjwa surua yaliripotiwa duniani, ikiwa ni ongezeko la asilimia 300 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Hapa Tanga, taarifa zinaonyesha kuwa mkoa umesonga mbele katika utekelezaji wa chanjo ya surua huku ikiripotiwa kuwa umeweza kupita lengo la asilimia 95 lililowekwa na Umoja wa Mataifa kwa asilimia tano.

Kaimu Mganga Mkuu wa Jiji la Tanga, Gidion Joshua anasema katika kila mwaka wa fedha, bajeti zao za afya wanatenga vifungu maalumu kwa ajili ya mafunzo kwa watoa huduma za afya kwa mama na mtoto.

Joshua anasema mafunzo hayo yana lengo la kuboresha afya hasa kuwa na lugha nzuri na namna ya kuhudumia kwa usahihi ili siku ambayo mzazi atapangiwa kurudi katika chanjo arejee kwa wakati.

Chanzo: mwananchi.co.tz