Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Haya ndio madhara ya dawa za binadamu zisipotumika kwa usahihi

Dawa Sumuuu Haya ndio madhara ya dawa za binadamu zisipotumika kwa usahihi

Sat, 17 Sep 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam (AKH,D) kwa kushirikiana na Chama cha Wafamasia Tanzania (PST) wameadhimisha siku ya usalama wa wagonjwa duniani huku wakitoa angalizo kuhusu matumizi holela ya dawa.

Wamesema mbinu zisizo salama za dawa na makosa ya dawa hasa kwenye matumizi ndiyo sababu kuu za madhara ambayo yanaepukika duniani kote.

Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu “Usalama wa dawa – Dawa bila madhara” yameenda sambamba na uzinduzi wa jarida maalum kama kiashiria cha  kuunga mkono jitihada ambazo zinaonyesha huduma wanazozitoa ni salama kwa hospitali na wateja wao.

Akizungumza katika halfa hiyo iliyofanyika jana Ijumaa Septemba 16, 2022 katika viwanja vya hospitali hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Tiba wa AKHS,T, Profesa Ahmed Jusabani amesema madhara ya dawa yanatokana na michakato ya upendekezaji, ushughulikiaji, utoaji, usimamiaji na ufuatiliaji wa dawa.

“Kaulimbiu ya mwaka huu ya “Dawa bila madhara” inaweka mkazo katika kuimarisha michakato hii na kuhakikisha matumizi yaliyo salama na yanayozingatia ubora ya dawa hizi.

“Kama mtoa huduma za afya katika jamii, AKHS,T inahimiza kuweka kipaumbele katika usalama wa dawa na kuchukua hatua za kupunguza madhara yanayohusiana na dawa,” amesema Profesa Jusabani.

Mganga Mkuu wa Mkoa, Dar es Salaam Dk Rashid Mfaume amesisitiza huduma zinazotolewa katika ngazi zizingatie viwango vinavyokubalika kama ilivyoagizwa na Wizara ya Afya na Baraza la Famasi Tanzania (PC) kuhusu ubora na hatua za usalama.

Amesema ubora na usalama wa wateja na watoa huduma za afya katika mchakato wa utoaji huduma ni kipaumbele cha Serikali.

Dk Mfaume ameushauri umma kuepuka tabia hatarishi kwa afya za watu kujiamulia kuhusu masuala ya huduma za afya ikiwemo kutumia dawa bila mapendekezo na ushauri wa tabibu.

Mkuu wa Wauguzi wa AKH,D Aika Mongi amesema “Tunahakikisha wauguzi wetu wana uelewa mpya kuhusu mbinu salama za dawa kupitia ukaguzi wa kila mwaka wa stadi za umahiri wa usimamiaji wa dawa.”

Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania(PST) Fadhili Hezekiah amesisitiza kwamba usalama wa wagonjwa ni muhimu sana kwa muktadha wa suala la kudhibiti viini sugu (AMR) ambalo ni Ajenda ya Kimataifa.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz